Michuano ya kufuzu kwa kombe la dunia

Mwenyekiti wa chama cha soka cha Ethiopia, Sahilu Gebremariam, amekiri kuwa walimtumia mchezaji aliyefungiwa kucheza na FIFA.

Gebremariam ameiambia BBC kwamba mchezaji huyo Minyahil Teshome Beyene angelikosa mchezo huo kutokana na kwamba alikuwa ameonyeshwa kadi mbili za njano katika mechi zilizotangulia.

Amesema hawatakata rufaa kwa kuwa kosa ni lao,na kwamba wamekubali hatua za kinidhamu za FIFA. Hii inamaanisha kwamba Ethiopia itaondolewa alama 3 ilizokuwa imepata iliposhinda Botswana mabao 3-0.

Hata hivyo bwana Gebremariam bado ana matumaini kuwa timu yake inaweza kusonga mbele katika hatua itakayofuata,kwa kuwa hata kama alama hizo zitaondolewa itasalia kwenye nafasi ya kwanza ikiizidi Afrika Kusini alama 2. Katika mechi za mwisho Ethiopia itakuwa ugenini dhidi ya Jamuhuri ya Afrika ya kati ilhali Afrika kusini itaipokea Botswana.