Nigeria waondolewa kombe la Mabara

Image caption wachezaji wa Nigeria wakishangilia ushindi dhidi ya Tahiti

Mabingwa wa Afrika, timu ya taifa ya Nigeria imeondolewa kwenye michuano ya kombe la mabara baada ya kutandikwa mabao 3-0 na mabingwa wa dunia Hispania.

Mabao mawili ya beki wa klabu ya Barcelona, Jordi Alba na moja la mshambuliaji wa Chelsea, Fernando Torres yalitosha kuzamisha jahazi la Nigeria ambao wameshinda mechi moja pekee dhidi ya Tahiti wikiendi iliyopita.

Nigeria wameyaaga mashindano hayo baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi B wakiwa na pointi tatu nyuma ya Uruguay walioko kwenye nafasi ya pili wakiwa na point sita.

Hispania ni vinara wa kundi B wakiwa wamemaliza hatua ya makundi na ushindi wa asilimia mia moja wakiwa na pointi tisa ambapo sasa watakwenda kuwavaa Italia katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo hapo siku ya siku ya alhamisi mjini Fortaleza.

Uruguay wao wametoa kipigo cha magoli 8-0 kwa timu wachovu kwenye michuano hiyo Tahiti ambao wameondoka na jumla ya magoli 24 ya kufungwa na kupata bao moja pekee walipocheza na Nigeria.

Kwa matokeo hayo, Uruguay watacheza nusu fainali dhidi ya wenyeji Brazil, hapo siku ya jumatano.