Soldado avunja rekodi ya usajili Spurs

Image caption Roberto Soldado

Tottenham Hotspur imevunja rekodi yake ya usajili kwa kulipa pauni millioni 26 kwa mshambuliaji Roberto Soldado kutoka klabu ya Valencia ya Hispania.

Mchezaji huyo wa umri wa miaka 28 amesaini mkataba wa miaka minne baada ya ukaguzi wa afya yake na anakua mchezaji wa tatu kusajiliwa na Spurs katika awamu hii ya usajili.

Soldado ameichezea Hispania mara 11 na amefunga mabao 30 katika mechi 46 alizoichezea Valencia katika msimu uliopita.

Soldado aliisaidia Hispania kufuzu fainali ya kombe la mabara mwezi uliopita, akichangia bao katika mechi dhidi ya Uruguay.

Alikua mchezaji wa akiba katika mechi ya fainali ambapo Brazil illibuka mshindi wa mabao 3-0.

Soldado anatazamiwa kuichezea Tottenham katika mechi ya mwisho ya kujipima nguvu dhidi ya Espanyol katika uwanja wa White Hart Lane siku ya Jumaamosi.

Rekodi ya zamani ya usajili kwa Spurs ilikua pauni millioni 17 ilipomsajili wiki chache zilizopita kiungo mchezaji Paulinho kutoka Corinthians ya Brazil .

Spurs pia imemsajili winga Nacer Chadli kutoka FC Twente kwa kulipa pauni millioni 7.

Soldado alizaliwa Valencia lakini alianza kuichezea Real Madrid,akifunga mabao 63 katika mechi 120 za ligi kwa timu ya pili ya Real Madrid Castilla.