Misri yaifunga Uganda 3-0

Image caption Mohamed Salah

Licha ya machafuko kuendelea nchini mwao, timu ya taifa ya Misri imeitandika Uganda The Cranes mabao 3-0.

Mabingwa wa kihistoria wa Afrika, wameifunga Uganda katika mchezo huo wa kirafiki uliopigwa kwenye uwanja El Gouna kilometa 430 kutoka mji wa Cairo ambako machafuko yametokea.

Ahmed Hassan Koka ambaye anakipiga kwenye klabu ya Rio Ave ya Ureno alifunga bao la kwanza kwa Mapharao katikati ya kipindi cha kwanza.

Bao la pili lilifungwa dakika 12 baada mapumziko na mfungaji bora wa michuano ya kufuzu kombe la dunia kwa kanda ya Afrika Mohamed Salah.

Ibrahim Salah alihitimisha ushindi wa Misri kwa kufunga bao la tatu.

Misri imecheza bila wachezaji wake wa timu za Al Ahly na Zamalek ambao wanajiandaa na mechi ya raundi ya pili ya klabu bingwa barani Afrika.

Mchezo huo kwa Uganda ulikuwa ni kwaajili ya kujiandaa na mechi muhimu ya kufuzu kombe la dunia dhidi ya Senegal nchini Morocco mwezi ujao.

Katika Mchezo mwingine wa Kirafiki, Malawi imeichapa Rwanda 1-0 katika mchezo uliochezwa mjini Kigali.