Man.City yaonyesha mchezo bora

Man City v Newcastle
Image caption Man City v Newcastle

Klabu ya Manchester City iliyocheza mechi yake ya kwanza msimu huu jumatatu usiku dhidi ya Newcastle United, ilionyesha ubora wake kuliko klabu zote zilizoanza mechi za msimu mpya.

Ushindi wa City wa 4-0 dhidi ya Newcastle haukuwa ni sababu wanacheza na vibonde, hata kidogo ni mipango ya Kocha mpya Manuel Pellegrini aliyebadili mchezo wa klabu hio.

Wachezaji wote walionyesha mori na tamaa ya kucheza na mabadiliko yaliyodhihirika ni mfumo tofauti na mwaka jana chini ya Roberto Mancini.

Mchezo ulikua wa pasi za uhakika na kila mpira ulipokua katikati mfano wa kiungo Yaya Toure utawaona wachezaji wengine wakijitahidi kupenya nyuma ya mabeki wa Newcastle.

Itakumbukwa na kama ilivyodhihirika tofauti iliyojitokeza ni kua wakati wa Mancini wachezaji walishughulika wakati wakiwa na mpira lakini chini ya Pellegrini utaona wakihangaika kuupokonya kutoka kwa wapinzani wao.

Mara kwa mara Man.City ilishindania mpira katika nusu ya Newcastle na sio upande wao. La kushangaza ni kwamba washambuliaji kama Edin Dzeko na Sergio Agueroa na baadaye Samir Nasri walizuia pasi za Newcastle katika upande wa upinzani.

David Silva na mchezaji mpya Jesus Navas walicheza kila mahali. Na kila walipomiliki mpira mwendo wao, uhakika wa pasi na kasi ziliwazidia wachezaji wa Newcastle na hata kabla ya Steven Taylor kuonyesha kadi nyekundu dakika 44 ya kipindi cha kwanza.

Pellegrini alitumia washambuliaji wawili Dzeko na Aguero lakini mfumo ulifanana na 4-3-3 kuliko ule wa 4-4-2 sababu Jesus Navas alimiliki upande wa kulia a kukaa mbele utadhani ni mshambuliaji huku upande wa pili wa shoto akiweko David Silva ambaye mara kwa mara alikua nyuma ya washambuliaji wawili.

Baada ya mechi hii, Kocha wa Newcastle Alan Pardew alieleza kua alikasirishwa na kitendo cha Arsenal kutangaza kumhitaji mcheza kiungo wa klabu yake mda mfupi kabla ya mechi kabambe kama hiyo.

Mabao ya David Silva, Sergio Aguero, Yaya Toure na Samir Nasri yaliipa City ushindi wa kuhakiki na kujieleza kuwa msimu huu wamepania kushinda siyo tu Ligi kuu ya England bali hata kutoa ushindani mkali barani Ulaya.

Pardew anasema kua hatua ya Arsenal kutangaza kua inamtaka Cabaye kabla ya mechi hiyo ilivuruga matayarisho yao.