Nani ndani, Fenerbahce au Arsenal?

Image caption Arsene Wenger kocha mkuu Arsenal

Baada ya kuanza vibaya msimu wa ligi kuu soka nchini England,

Arsenal usiku wa leo jumanne itajitupa uwanjani kuvaana na Fenerbahce ya Uturuki katika mchezo wa mtoano wa kuwania kushiriki michuano ya klabu bingwa barani Ulaya.

Arsenal itacheza bila ya kiungo wake Alex Oxlade-Chamberlain.

Kinda hilo wa miaka 20 anasumbuliwa na jeraha la goti alilolipata wakati timu yake ikitandikwa 3-1 nyumbani na Aston Villa.

Bosi wa The Gunners, Arsene Wenger amethibitisha kuwa nyota huyo hatoweza kurejea uwanjani kwa takribani wiki sita.

Mabeki Bacary Sagna, Kieran Gibbs and Nacho Monreal wote wanatarajia kuwemo kwenye kikosi cha Arsenal usiku huu.

Mshindi katika mechi mbili hizo ambazo zitachezwa nyumbani na ugenini atapata nafasi ya kuwemo kwenye hatua ya makundi ya klabu bingwa Ulaya msimu ujao.

Arsenal inacheza mechi hiyo kutokana na kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimu wa ligi kuu nchini England na haijawahi kukosa hatua ya makundi ya klabu bingwa ulaya kwa miaka 14 mfululizo.

Lakini kuanza vibaya kwa mechi yao ya ligi kunawatia mashaka mashabiki wa klabu hiyo.

"tulipambana sana kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye ligi msimu uliopita, na mechi hii ina umuhimu mkubwa kwetu" Amesema kocha wa Arsenal, Arsene Wenger.

Fenerbahce,wanashiriki hatua ya michuano hii ilihali bado wanakabiliwa na kifungo cha kutoshiriki michuano yoyote ya Ulaya baada ya kukutwa na kashfa ya kupanga matokeo,lakini rufaa waliyokata inawapa nafasi ya kuendelea kushiriki michuano hiyo.

Rufaa yao itasikilizwa tarehe 28 mwezi wa nane, Siku moja baada ya kufanyika kwa mechi ya marudiano.

Uwamuzi wa rufaa hiyo huenda ukawa na manufaa kwa Arsenal kama wakipoteza mechi hiyo.