Cape Verde yaadhibiwa na FIFA

Image caption Kikosi cha Cape Verde hakitashiriki mchuano wa kombe la dunia mwaka 2014

Cape Verde imebanduliwa nje ya kinyanganyiro cha kufuzu kwa dimba la dunia Mwakani kwa nchi za Afrika. Kwa mujibu wa tovuti ya shirikisho la soka duniani FIFA, Cape Verde ilikosea kwakumshirikisha mchezaji aliyekuwa amepigwa marufuku katika mechi yao dhidi ya Tunisia Jumamosi iliyopita

Kwa mujibu wa FIFA Fernando Verela hakufaa kucheza katika mechi hiyo waliyoshinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Tunisia . FIFA sasa imebadilisha matokeo hayo na kuipa Tunisia ushindi mkubwa wa mabao 3-0 .

Kauli hiyo imeipa Tunisia alama za kutosha kuipiku Cape Verde kutoka kileleni mwa kundi B ikiwa na alama 14 .Cape Verde ni ya pili na alama 14.

Shirikisho la soka la Cape Verde lilimetozwa faini ya dola $ 6400 .Sadfa ni kuwa Cape Verde ilinufaika na alama za bwerere mapema mwakani Equatorial Guinea ilipoadhibiwa kwa kumshirikisha mchezaji kinyume na sheria za FIFA za uraiya wa wachezaji.

The Blue Sharks ya Visiwa vya Cape Verde walikuwa wamelazwa mabao 3-4 na Equatorial Guinea lakini FIFA ikabadilisha matokeo hayo kwani Emilio Nsue Lopez hakutimiza kanuni za uraiya wa taifa hilo .

Sasa Tunisia ndiyo itakayosonga mbele katika raundi ya mwisho itakayochezwa katika droo itakayofanyika Jumatatu tarehe 16.