Ghana kukutana na Misri kutafuta nafasi Brazil

Image caption Mashabiki wa soka Ghana wanatumai kuwa nchi yao itafuzu Brazil 2014

Ghana itamenyana na Misri katika mechi za kuamua nchi ya Afrika itakayowakilisha bara zima katika dimba la kombe la dunia mwaka ujao nchini Brazil.

Misri kama nchi pakee ambayo imeshinda mechi zake zote za makundi za kufuzu kushiriki kombe la dunia, bila shaka imeitia hofu nchi zengine na bila shaka hakuna ambaye angependa kukukutana nao.

Hii ni kutokana na matokeo ya draw iliyofanywa ambapo mataifa ya kiafrika zitacheza kwenye michuano ya kutafuta mwakilishi wa bara la Afrika Brazil mwaka ujao.

Mabingwa wa Afrika Nigeria watachuana na Ethiopia wakati Ivory Coast wakitoana jasho na Senegal.

Tunisia, waliofuzu baada ya Cape Verde watachuana na Cameroon.

Burkina Faso, nao waliomaliza wa pili katika michuano ya taifa bingwa Afrika watatoana jasho na Algeria.

Mechi za awamu ya kwanza ya michuano hiyo, zitachezwa kati ya tarehe 11 na 15 Oktoba, huku mechi za marudio zikichezwa kati ya tarehe 15-19 Novemba.

Shirikisho la soka duniani, Fifa, limezitaka nchi hizo kuchagua tarehe za mechi, eneo wanalotaka kuchezea mechi yao ya kwanza ifikapo Ijumaa wiki hii.

Wakati Ghana wanahisi kutokuwa na bahati baada ya kuamuliwa kuwa watacheza na Misri, wanaweza kujipa moyo kwani waliwahi kuwashinda Misri kwenye mechi ya kirafiki iliyochezwa Dubai mwezi Januari.

Na haijulikani ikiwa Misri watacheza mechi yao ya marudio mjini Cairo kwani mgogoro wa kisiasa unatokota nchini humo.