Wilshere:Waingereza tu waichezee England

Image caption Wilshere huchezea klabu ya Arsenal

Mchezaji wa kiungo wa Arsenal na England amezusha mjadala kuhusu matamshi yake kwamba Waingereza tu ndio waiwakilishe timu ya soka ya England.

Jack Wilshere alikua akielezea msimamo wake baada ya kijana wa Manchester United Adnan Januzaj kutajwa kwamba anaweza kuichezea England ikiwa atatimiza masharti ya Fifa ya ukaazi wa miaka 5 kwa kua bado hajaamua alichezee taifa gani.

Januzaj, mwenye umri wa miaka 18, ana haki ya kuchezea Ubelgiji, Serbia, Albania na Uturuki.

Alipoulizwa kuhusu hilo , Wilshere alijibu: "Kuishi England kwa miaka mitano haikufanyi kua Muingereza."

Baadae akiandika katika mtandao wa jamii wa Twitter alisema matamshi yake hayakumkusudia Januzaj. "swali lilikua wachezaji wageni waruhusiwe kuichezea England, na kwa maoni yangu sidhani waruhusiwe. Yeye ni mchezaji hodari lakini si Muingereza."

Kocha wa England Roy Hodgson amethibitisha amekua akimchunguza Januzaj."Nikienda Hispania na kuishi huko kwa miaka mitano sitachezea Uhispania.."

Mchezaji wa Liverpool Raheem Sterling, aliyezaliwa Jamaica, na Wilfried Zaha wa Manchester United,aliyezaliwa Ivory Coast, wanachezea timu ya England ya umri wa miaka 21 pamoja na Saido Berahino, aliyekimbia Burundi akiwa na umri wa miaka 10.