Bale ni kati ya wanaowania tuzo ya Fifa

Gareth Bale
Image caption Bale aliandikisha rekodi mpya ya mchezaji soka kununuliwa kwa pesa nyingi zaidi duniani.

Gareth Bale, mchezaji aliyeandikisha rekodi ya kununuliwa kwa bei ya juu zaidi duniani, ni miongoni mwa wachezaji 23 wanaoshindania tuzo ya Fifa ya mchezaji bora zaidi.

Bale, kutoka Wales, na mwenye umri wa miaka 24, aliifungia Tottenham magoli 26 msimu uliopita, kabla ya kununuliwa na Real Madrid kwa kitita cha pauni milioni 85.

Kati ya wachezaji wengine wa ligi kuu ya Premier waliopo katika orodha fupi ya wachezaji wenye matumaini ya kulinyakua tuzo la Ballon d'Or ni pamoja na Eden Hazard, Mesut Ozil, Luis Suarez, Yaya Toure na Robin van Persie.

Mchezaji wa Barcelona, Lionel Messi, pia naye ana matumaini ya kulipata tuzo hilo, ambalo ameshinda kwa miaka minne mfululizo iliyopita.

Wachezaji wenzake wenye matumaini ni pamoja na Andres Iniesta, Neymar, aliyejiunga na timu hiyo ya Nou Camp kutoka Santos, na vile vile Xavi.

Cristiano Ronaldo wa timu ya Real Madrid pia yumo.

Mshambulizi wa Manchester United, Wayne Rooney, mwaka jana jina lake lilikuwepo katika orodha fupi, lakini mwaka huu halipo.

Bayern Munich ya Ujerumani ambayo iliishinda Barcelona katika juhudi za kuwa bingwa barani Ulaya, ina majina ya wachezaji sita katika orodha fupi.

Majina hayo 23 yatapunguzwa hadi majina matatu mwezi Desemba, kabla ya mshindi kutangazwa mjini Zurich, Uswisi, tarehe 13 mwezi Januari, mwaka 2014.

Kocha wa zamani wa Bayern, Jupp Heynckes, ambaye wadhifa wake ulichukuliwa na Pep Guardiola, naye ana matumaini ya kutajwa kama mshindi wa tuzo ya kocha bora zaidi wa mwaka.

Meneja wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, Jose Mourinho wa Chelsea na Rafael Benitez wa Napoli, wote watashindania tuzo hiyo ya kocha bora zaidi, katika orodha ya majina ambayo ina makocha kumi.