Morsi amponza Bingwa wa Kung Fu Misri

Image caption Rais aliyeondolewa madarakani, Mohamed Morsi

Bingwa wa mchezo wa Kung fu nchini Misri, Mohammed Youssef amevuliwa medali yake ya dhahabu baada ya kuonesha ishara ya kumuunga mkono Rais wa Misri aliyeondolewa madarakani, Mohamed Morsi.

Youssef alipigwa picha katika mashindano nchini Urusi akiwa amevaa T-shirt yenye alama yenye kuonesha ushirikiano na Waandamanaji wanaomuunga mkono Morsi.

Serikali ya Misri imekuwa ikipambana na waandamanaji tangu baada ya Morsi kuondolewa madarakani mwezi Julai.

Kaka wa mwanamichezo huyo Hammam amesema Youssef alirudishwa nyumbani kutoka kwenye mashindano hayo na kuhojiwa alipowasili nchini mwake.

Mkurugenzi wa chama cha Kung Fu nchini Misri, Gamal El-Jazzar amesema Youssef atafungiwa kuiwakilisha Misti kwenye michuano ya dunia ya mchezo huo, hata hivyo haijafahamika kama atafungiwa moja kwa moja.