Arsenal,Chelsea, Barca shwari Uefa

Image caption Aaron Ramsey kulia akishangilia bao na Santi Cazorla

Timu za Arsenal na Chelsea za England zimejiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu kucheza kumi na sita bora kuwania kombe la Uefa.

Bao pekee la Aaron Ramsey lilitosha kuipa Arsenal pointi tatu muhimu dhidi ya Borussia Dortmund ya Ujerumani na hivyo kujikusanyia pointi 9 katika kundi lake F na hivyo kuongoza wakiwa sawa na timu ya Napoli ya Italia.

Ramsey alifunga bao hilo katika dakika ya 62. Dortmund wanashikilia nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi sita, huku Marseille ya Ufaransa ikishikilia mkia bila pointi. Katika mchezo mwingine Chelsea ilijipatia pointi tatu kwa kuiadhibu timu ya Schalke 04 ya Ujerumani kwa jumla ya magoli 3-0. Mabao ya Chelsea yalitumbukizwa na Samuel Etoo magoli mawili huku De Mbamba akiifungia timu yake ya Chelsea goli la tatu. Nayo Barcelona imefanya kile kilichotarajiwa na mashabiki wake baada ya kuiadhibu AC Milan ya Italia magoli 3-1. katika magoli hayo ya Barcelona, Messi aliweka kimiani magoli mawili huku lingine likifungwa na Sergio Busquets. Goli la AC Milan lilikuwa la kujifunga kwa mlinzi wa Barcelona Gerard Pique. Kwa timu za England, Manchester City tayari imefuzu kucheza ngazi ya makundi ya 16 bora pamoja na Bayern Munich katika kundi lao, kwani hakuna timu nyingine ya kundi hilo itakayozipiku pointi za timu hizo mbili.