John Mikel Obi

Imebadilishwa: 12 Novemba, 2013 - Saa 04:31 GMT

Akiwa mchezaji wa timu ya Chelsea ya England kwa miaka saba, John Mikel Obi amecheza mechi 187 na kushinda makombe kadhaa, likiwemo la ubingwa wa Ligi Kuu ya England, Kombe la Mabingwa barani Ulaya na makombe manne ya chama cha mpira cha England, FA.

Angaliweza kuwa mchezaji wa Manchester United, wakati huo klabu hiyo ya Old Trafford walifikiri wangemsajili mchezaji huyo kutoka klabu ya Lyn Oslo ya nchini Norway wakati huo John Mikel akiwa na umri wa miaka 18. Hata hivyo, baada ya mvutano kuhusu suala lake, hatimaye klabu ya Chelsea ikafanikiwa kumsajili mchezaji huyo kinda mwezi Juni 2006.

Tangu wakati huo, Mikel hajaweza kukengeuka kuhusu timu yake na hivyo kujijengea uwepo wake wa mara kwa mara katika kikosi cha Chelesea the Blues na kikosi cha taifa cha Nigeria-kwa kuichezea nchi yake mara 51 na kusaidia kuipatia ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika mapema mwaka huu.

Mikel ni mchezaji mzuri katika nafasi ya kiungo na mwenye nidhamu awapo mchezoni, na ilimchukua Mikel hadi mwezi Septemba mwaka huu kufunga bao lake la kwanza kwa timu yake ya Chelsea katika Ligi Kuu ya England, akiichezea timu hiyo mara 185, katika mechi hiyo Chelesea ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fulham.

Labda kiwango chake cha juu kabisa alikionyesha mwaka 2012 katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Bayern Munich, ambapo Mikel alionyesha mchezo wa kiwango cha juu katika nafasi ya kiungo mlinzi na kusaidia timu yake kupata sare ya 1-1 baada ya dakika 120 za mchezo mkali uliomilikiwa na miamba hiyo ya Ujerumani. Chelsea waliendelea kupigana na kuingia katika hatua ya mikwaju ya penalti. Na ndipo waliposhinda na kunyakua kombe hilo, wakiwa chini ya uongozi wa kocha Roberto Dimateo.

Umuhimu wa Mikel katika kikosi cha Chelsea ni kwamba mwaka jana aliongeza mkataba wa miaka mitano kuicheza klabu hiyo, hivyo kumaanisha atakuwepo Stamford Bridge hadi mwaka 2017.

Tathmini kumhusu Obi Mikel

Baada ya Nigeria kutwaa ubingwa mwaka 2013, huu umekuwa mwaka ambao John Mikel Obi amedhihirisha kuwa mmoja wa wachezaji mahiri kabisa barani Afrika.

Hakuna mchezaji yeyote barani Afrika ambaye amepata mafanikio makubwa mwaka huu kama mchezaji huyu wa Nigeria, ambaye aliuanza msimu huu kwa mafanikio makubwa na kwenda mbele zaidi.

Kufanikiwa kwa Mikel katika kusakata kandanda kumekuwa na mwelekeo mzuri lakini pia akikabiliana na changamoto kadha. Miaka mingi ya kucheza nafasi ya ulinzi katika klabu yake ya Chelsea, kumepunguza kasi yake ya kuwa mchezaji mshambuliaji katika timu yake ya taifa ya Super Eagles.

Ufanisi wake katika timu ya Nigeria katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2013, kulienda mbali zaidi kuwakumbusha mashabiki mchango wake katika nafasi ya ulinzi.

Katika mashindano yaliyofanyika Afrika Kusini, alikuwa mmoja wa wachezaji wakongwe wa klabu hiyo, akiwa na umri wa miaka 25 tu na kupewa majukumu ya kuwa mshambuliaji kiungo tofauti na nafasi ya kiungo mlinzi anayochezea katika klabu yake ya Chelsea.

Nigeria ilishinda Kombe la Mataifa ya Afrika, Mikel akiwa mchezaji katika mecho zote. Nigeria, Super Eagles waliwalaza Burkina Faso bao 1-0 katika mchezo wa fainali.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.