Pierre Emerick Aubameyang

Image caption Pierre Emerick anasakata soka yake barani Ulaya

Akiwa mchezaji wa zamani wa timu ya vijana ya AC MILAN, soka la Pierre Emerick Aubameyang lilianza kuchomoza baada ya kujiunga na klabu ya Saint Etienne kwa mkataba wa kudumu mnamo mwaka 2011.

Lakini mkataba huo ulimalizika Julai baada ya kujiunga na washindi wa pili wa Kombe la Klabu Bingwa Barani Ulaya, Borussia Dortmund , akichukua nafasi ya Mario Gotze, baada ya uhamisho wake uliotarajiwa sana kwenda Bayern Munich.

Lakini mkataba wake na Les Verts ulimalizika kwa mtindo wa aina yake, kwani kalbu hiyo ilishinda taji la French League One kwa mwaka 2013, hivyo kumwezesha Aubameyang , kupata tuzo yake ya kwanza kama mchezaji wa kulipwa.

Ingawa hakufunga goli katika mchezo huo, lakini aliwahi kuzifumania nyavy mara 19, katika ligi kuu ya Ufaransa , huku mchezaji wa PSG, Zlatan Ibrahmovic, akiongoza kwa mabao, na mchezaji huyo kutoka Gabon akiwa ametoa pasi nane zilizozaa mabao.

Uchezaji huo mahiri ndio ulioishawishi Dortmund, kumnunua kwa kitita cha Paundi milioni 11 kwa mkataba wa miaka mitano.

Na mara alijiongezea tuzo, baada ya Dortmund kulipiza kisasi cha kufungwa katika fainali ya Klabu Bingwa Barani Ulaya jijini London mnamo Mei, kwa kuwafunga mahasimu wao Bayern Munich mabao 4 -2 hivyo kutwaa taji la Supercup la ufunguzi wa msimu wa Ligi Kuu ya Ujerumani.

Aliibuka na kuwa mchezaji wa sita kufunga mabao matatu peke yake yaani ‘Hat Trick’ katika mchezo wake wa kwanza akiwa na Dortmund ilipocheza na Ausburg na kuifunga mabao 4 – 0.

Magoli yaliendelea kutiririka huku Aubameyang akijipanga vilivyo hasa kutokana na kuzifumania nyavu mara saba katika mechi 11 alizocheza katika klabu inayofundishwa na Jurgen Klopp.

Wakati soka lake kwa upande wa klabu liliendelea kukua kwa mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 24, mwaka 2013 ulikuwa si wa kuridhisha upande wa kimataifa.

Hata hivyo, mwanga ulichomoza tena pale alipopachika ‘Hat Trick’ kwa njia ya penalty dhidi ya Niger katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia mnamo mwezi Juni, lakini huo ulikuwa ushindi pekee wa timu ya taifa ya Gabon maarufu kama ‘Panthers’ na kushika nafasi ya tatu katika kundi lao, hivyo kufuta matumaini ya kushiriki Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Brazil mnako 2014.

Maoni ya wadadisi wa soka kumhusu Emerick

Mshambuliaji huyo wa Gabon alifunga ‘Hat Trick’ dhidi ya klabu ya Augsburg katika mechi ya ufunguzi ya msimu mpya na kudhiirisha moja kwa moja kwa mashabiki kwamba, alistahili kununuliwa kwa Paundi milioni 11 na kujiunga na klabu hiyo ya Ujerumani.

Huo kimsingi utakuwa ulikuwa mwaka muhimu kwa mshambulijai huyo mwenye miaka 24

Mnamo mwaka 2012, alivutia katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, iliyofanyika nchini mwake na baada ye alighairi kujiunga na Tottenham Hotspur.

Hivyo 2013, Aubemeyang alilazimika kudhiirisha kwamba, anaweza kufikia kiwango cha juu , na kweli alifanya hivyo .

Bao lake la St Etienne, katika ushindi wa timu yake wa mabao 3 – 0 dhidi ya Bastia mnamo Januari, ulikuwa ni mwanzo wa mfululizo wa kupachika mabao ambao ulimfanya azifumanie nyavu katika mechi saba za Ligi Kuu ya Ufaransa.

Aubameyang alimaliza msimu akiwa amepachika mabao 19 katika ligi, na pia alitoa pasi iliyozaa bao la ushindi katika fainali ya Kombe la Ligi la Ufaransa, baada ya St – Etienne kushinda kombe muhimu baada ya miaka thelathini.

Alihusishwa na kujiunga na klabu kubwa katika majira ya jotona mengi yanasemwa kuhusu kiwango chake cha usakataji kabumbu, na kwamba, Borussia Dortmund, timu ambayo iliifunga Real Madrid ili kufikia fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Ulaya, ilipambana vilivyo kupata saini ya mwanandinga huyo.

Inawezekana Aubameyang hapangwi katika kikosi kinachoanza pale timu yake inapocheza kwa sasa, lakini Jurgen Klopp, mpishi wa mafanikio ya Dortmund, anasema tayari ameonesha mafanikio makubwa na kuvutia, katika moja ya vilabu vyenye kipaji Barani Ulaya.

Moja ya mafanikio hayo ni pamoja na kufanikiwa kukimbia muda wa haraka zaidi kwa mita thelathini kuliko bingwa wa mbio za mita 100 duniani Usain Bolt.

Licha ya juhudi kubwa za Aubameyang, timu ya taifa ya Gabon imeshindwa kuonesha cheche kwa mwaka 2013, lakini kwa upande wa klabu umekuwa ni mwaka wa mafanikio kwa mshambuliaji huyo.

Na hivyo basi nitampigia kura kuwa Mwanasoka Bora wa Afrika wa BBC kwa mwaka 2013.