Jeraha lamzonga Andre Ayew

Image caption Andre Ayew

Mwanakandanda wa timu ya taifa ya Ghana Andre Ayew hataweza kucheza kwa takriban kipindi cha majuma manane baada ya kutegua goti.

Kijana huyo wa umri wa miaka 23 aliumia goti lake wakati wa pambano la mkondo wa pili dhidi ya Misri katika kinyang'anyiro cha nafasi za fainali ya kombe la dunia siku ya jumaanne.

Klabu yake ya Marseille ya Ufaransa ilisema katika wavuti wake kwamba Ayew alipimwa na madaktari na kupatikana ametegua goti lake na atafanyiwa operesheni siku ya Jumaatatu.

Hili ni pigo kubwa kwa Ayew, ambae amekua akitamba katika michezo ya hivi karibuni na akifunga mabao manne katika michuano tisa aliyokwishacheza.

Ghana ilipoteza mechi ya mjini Cairo 2-1 lakini ikafaulu kucheza katika michuano ya fainali ya kombe la dunia nchini Brazil hapo mwakani kw akuibuka na ushindi wa jumla ya mabao7-3.