Tanzania yaingia robo fainali CECAFA

Image caption Timu ya taifa ya Tanzania

Timu ya taifa ya Tanzania bara "Kilimanjaro Stars" imesonga mbele hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati CECAFA Senior Challenge baada ya kuisambatisha timu ya Taifa ya Burundi "Intamba mu Rugamba" kwa goli 1 - 0.

Goli la Tanzania limefungwa dakika ya 8 kipindi cha kwanza na Mbwana Samatta mshambuliaji wa timu hiyo anachezea Klabu ya TP Mazembe ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa matokeo hayo ya mchezo huo wa kundi A unaifanya Tanzania bara sasa kufikisha pointi 7 baada ya kushinda mechi mbili na kutoka sare mmoja.

Tanzania ilitoka sare na Zambia ya goli 1 - 1 katika mchezo wa ufunguzi siku ya Alhamis iliyopita ambapo baadae iliifunga Somalia goli 1 - 0 mechi iliyopigwa siku ya jumapili kabla ya kushinda mechi kati yake na Burundi ya goli 1 - 0.

Katika mchezo mwingine wa kundi A Zambia walitarajiwa kupambana na Somalia.