Kenya na Sudan kumenyana fainali cecafa

Image caption Timu ya Kenya, Harambee Stars

Timu za Kenya na Sudan zimefuzu kucheza fainali za Shirikisho la Kandanda kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, CECAFA mwaka 2013.

Katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali uliochezwa uwanja wa manispaa Mombasa kati ya Sudan na Zambia, Sudan ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1.

Nayo Kenya, iliweza kujipatia bao la mapema kabisa katika dakika ya tano ya mchezo, wakati walipopambana na Kilimanjaro Stars ya Tanzania. Hivyo hadi mwisho wa mchezo, Harambee Stars ilikuwa imepata ushindi huo wa bao 1-0.

Mchezo kati ya Tanzania na Kenya ambao awali ulikuwa ufanyike katika uwanja wa Machakos, ulihamishiwa katika uwanja wa Nyayo mjini Nairobi, kutokana na uwanja wa Machakos kuwa katika hali mbaya baada ya mvua kubwa kunyesha.

Timu ya Tanzania na Zambia zitakutana katika mchezo wa kumpata mshindi wa tatu. Kuingia nusu Fainali Tanzania iliwatoa mabingwa watetezi the Cranes ya Uganda huku Zambia ikiwaondoa Burundi. Katika hatua hiyo pia Kenya waliweza kuwacharaza Rwanda, huku Sudan ikiwavurumisha Ethiopia nje ya michuano hiyo maarufu kwa kanda ya Afrika Mashariki. Zambia ni timu waalikwa katika mashindano hayo.