Suarez asaini kubakia Liverpool

Image caption Luis Suarez

Hatimaye Mshambuliaji mahiri wa Klabu ya Liverpoool Luis Suarez amesaini mkataba kuendelea kusakata Kabumbu kwenye Klabu hiyo yenye makao yake makuu Anfield.

Awali mkataba wa Suarez ambaye alijiunga na klabu hiyo January 2011 na akiwa tayari amekwishafunga mabao 17 msimu huu, ulitaraji kukamilika mwaka 2016.

“Nimefurahi kufikia makubaliano ya kuendelea kuitumikia kwa muda mrefu klabu hii ya Liverpool,tuna wachezaji mahiri klabuni hapa,na timu yetu inazidi kuimarika kila wakati,amenukuriwa akisema mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26”

“Ninaamini kuwa ninaweza kufikia malengo yangu kwa kutwaa mataji na kucheza kwa kiwango kikubwa nikiwa na kikosi cha Liverpool,lengo ni kujaribu kusaidia kufikia malengo hayo haraka kadri inavyowezekana”

Uhusiano kati ya Suarez na watendaji wakuu wa Liverpool umeimarika kwa kasi tangu alipojaribu kulazimisha uhamisho kwenda klabu ya Arsenal mwishoni mwa msimu uliopita.

Naye kocha mkuu wa klabu ya Liverpool Brendan Rodgers ameuambia mtandao wa klabu hiyo kuwa hiyo ni habari njema kwa kila mdau wa Klabu ya Liverpool,wakiwemo wamiliki wa klabu lakini muhimu Zaidi Mashabiki wa klabu hiyo.

Luis ni mchezaji wa kiwango cha Dunia mwenye kipaji cha hali ya juu,na kwa kuendelea kuwa naye wakati huu ni jambo la msingi katika kile tunacholenga kukipata hapa klabuni kwetu.

Jambo muhimu na la kusisimua ni kwamba ndiyo kwanza ana umri wa miaka 26,na ni wazi kwamba tutaendelea kumshuhudia ubora wake siku zijazo,akiwa ndani ya jezi za Liverpool.