Kocha wa Cardiff afutwa Kazi

Image caption Malky Mackay

Sakata kuhusu hatma ya kocha Malky Mackay katika klabu ya Cardiff, imefika kikomo baada ya klabu hiyo kuthibitisha kuwa amefutwa kazi.

Kufutwa kwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 42, kulikuwa kumebashiriwa, baada ya mmiliki wa klabu hiyo Vincent Tan, kumtumia barua pepe wiki iliyopita kumtaka ajiuzulu au afutwa kazi.

Hata hivyo, onyo hilo lilifutiliwa mbali baada ya mwenyekiti wa klabu hiyo Mehmet Dalman kutangaza kuwa kocha huyo atasalia, kwa muda usiojulikana, lakini baada ya Cardiff kunyukwa magoli matatu kwa bila na Southampton siku ya Alhamisi, mechi hiyo imegeuka na kuwa ya mwishi kwa kocha huyo wa zamani wa Watford.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na wasimizi wa klabu hiyo siku ya Ijumaa, kocha huyo sasa amefutwa kazi rasmi.

Taarifa hiyo imesema kuwa kocha mpya atateuliwa hivi karibuni.