Timu mbili Ligi ya Malawi zafungiwa

Image caption Wachezaji wa timu ya Silver Strikers ya Malawi

Vilabu viwili vya mpira wa miguu nchini Malawi vya Mighty Wanderers na Silver Strikers vimefungiwa kufuatia ghasia za mashabiki katika mchezo wao wa Desemba 28 mwaka jana.

Shabiki mmoja aliuawa na 20 kujeruhiwa katika uwanja wa Balaka, na mechi hiyo kufutwa.

Silver Strikers wamefungiwa kwa miezi minane na kutozwa dola za Kimarekani 6640.00, wakati ambapo timu ya Mighty Wanderers wamefungiwa kwa miezi mitano na kupigwa faini ya dola za Kimarekani 1620.00.

Timu hizo zinaweza kukata rufaa dhidi ya adhabu hiyo lakini zikiwa zimetoa kiasi cha dola $1046 katika muda wa saa 48 tangu kutolewa kwa adhabu hiyo.

Image caption Timu ya Mighty Wanderers ya Malawi

Kamati ya nidhamu ya ligi ya Malawi imezipata timu zote mbili kuwa na hatia kwa kushindwa kudhibiti vitendo vya mashabiki wao kinyume na kanuni za Fifa na hivyo kusababisha mchezo wa soka kuwa vurugu.

Silver Strikers nao walipatikana na hatia kwa kuchochea ghasia zilizosababisha kufutwa kwa mchezo huo, ukiwa katika dakika ya 61, wakati ambapo Mighty Wanderers FC ilishindwa kutoa ulinzi wa kutosha kwa timu ngeni ya Silver Strikers pamoja na watazamaji.

Katika taarifa hiyo, Ligi ya Malawi, "Super League of Malawi" wamesema kuwa adhabu hizo zimekuwa kali kwa sababu timu hizo mbili zimekuwa zikijirudia kutenda makosa.

Chombo hicho pia kimeamuru timu zote mbili kurudia mchezo huo bila kuwa na watazamaji, kabla ya tarehe 4 Januari, adhabu zao zitakapoanza kutekelezwa.

Hata hivyo, Silver Strikers wameonyesha kuwa watacheza mchezo wa marudiano iwapo tu utaanzia pale ulipoishia, yaani dakika ya 61 wakati walipokuwa wakiongoza kwa bao 1-0.