Familia ya soka yampoteza gwiji Eusebio

Eusebio
Image caption Eusebio enzi zake uwanjani.

Gwiji wa soka kutoka taifa la Ureno, Eusebio amefariki dunia.

Alikuwa na miaka 71 na kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya moyo.

Eusebio alizaliwa nchini Msumbiji kama Eusebio da Silva Ferreira na anatajwa kama mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea duniani.

Aliitumikia klabu ya mjini Lisbon,Benfica FC kwa miaka 22 ambapo uwezo wake wa mbio na kasi, kuutumia vyema mguu wake wa kulia na mbinu za kimpira kulimpa umaarufu sana nchini Ureno na kubatizwa jina la The Black Pearl or the Black Panther.

Wakati wa uchezaji wake alifunga mabao 733 katika mechi 745, pia alifunga mabao tisa kwenye michuano ya kombe la dunia ya mwaka 1966 na kuwa mfungaji bora wa mashindano hayo na kuisaidia Ureno kushika nafasi ya tatu kwenye michuano hiyo.