Wanariadha wa Kenya kutozwa Kodi

Haki miliki ya picha PA
Image caption David Rudisha

Wanariadha wa Kenya wameapa kupinga mpango wa serikali wa kuwalazimisha kulipa kodi kutokana na mapato yao.

Siku ya Jumanne, Shirika la utozaji ushuru nchini Kenya KRA lilitangaza kuwa mapato yote watakayoshinda wanariadha, ikiwa ni pamoja na wachezaji wa soka nje na ndani ya nchi ni sharti yatozwe ushuru kuanzia mwezi huu.

Lakini wanamichezo hao ambao huchangia kiasi kikubwa cha mapato yao katika uchumi wa taifa, wametishia kususia mashindano yote ya kimataifa ikiwa serikali itaendelea na mpango huo wa kuwatoza ushuru.

Wanariadha hao wamesema fedha wanazopata sio nyingi kwani huwa hawashindi hela kila mwezi na huenda ikawachukua zaidi ya miaka mitano kujiinua tena ikiwa serikali itawatoza ushuru.

Wakiongea mjini Eldoret, Magharibi mwa Kenya wanariadha hao, wakiongozwa na mbunge wa Cherangani ambaye pia ni bingwa wa zamani wa mbio za Boston Marathon Wesley Korir,wanadai kuwa KRA haina mfumo dhabiti wa kubaini kiasi cha fedha walizoshinda wanariadha, kwa sababu shirika hilo halijaorodhesha mbio walizo shiriki na kiasi cha fedha walizoshinda.

Mwaka wa 2012, wanariadha kadhaa akiwemo mshikilizi wa rekodi ya dunia wa mbio za mita mia nane kwa upande wa wanaume David Rudisha, bingwa mara mbili wa dunia wa mbio za Marathon Abel Kirui, walikabithiwa nyaraka na KRA kuwataka kulipa malimbikizi ya kodi inayokisiwa kuwa mamilioni ya madola.