Li Na atwaa Grand Slam ya pili

Haki miliki ya picha AP
Image caption LI Na akiwa na taji lake la Australian Open

Pengine sasa imeandikwa kwenye vitabu vya rekodi za dunia kuwa, Li Na raia wa uchina amekuwa mtu kwanza kutoka barani Asia kunyakuwa taji la michuano ya wazi ya Australia ijulikanayo kama Australian Open kwa mchezaji mmoja mmoja.

Li Na ameweza kuingia kwenye kumbukumbu hiyo muhimu baada ya mapema jumamosi kunyakuwa taji la pili ya Grand Slam ama michuano yenye hadi ya juu katika mchezo wa tenesi.

Alimfunga Mslovakia Dominika Cibulkova kwa seti tatu,ikiwa ni kwa pamoja 7-6 (7-3) 6-0.

Ikiwa ni fainali yake ya tatu ya michuano ya Grand Slam baada ya kuingia kwenye fainal mbili na kushinda moja hapo awali, sasa amekuwa mtu wa kwanza kutoka bara la Asia kucheza fainal tatu na kunyakuwa ubingwa mara mbili.

Taji lake la kwanza la Grand Slam alishinda mwaka 2011 kwenye michuano ya tenesi ya wazi ya Ufaransa maarufu kama French Open, kisha akacheza fainal ya michuano ya Australian Open mwaka jana ambapo aliingia fainal lakini akapoteza.

Sura yake iliishakuwa maarufu kwenye viwanja vya Melbourne Park kunakofanyika michuano hiyo inayofikia tamati hapo jumapili kwa fainal ya wanaume.

Akizungumza baada ya ushindi wake, Li alisema "hatimaye nimelipata, fainali mbili zilizopita ilikuwa karibu sana nishinde." Alisema Li Na mwenye umri wa miaka 31.

"Kwa sasa nashukuru jopo langu la ufundi, asante kwa wakala wangu kwa kunifanya kuwa tajiri,namshukuru sana. "

Aliongeza kwa kumshukuru mume wake ambaye alikuwa kwenye jukwaa akimshuhudia, alimwambia " Asante sana, wewe ni mume mwema. Pia una bahati."

Kwa upande mshindi wa pili wa michuano hiyo, Cibulkova alisema anashukuru hii ni fainal yake kwanza michuano mikubwa ya Grand Slam hivyo anashukuru jinsi alivyoweza kumudu mchezo huo.

Wachambuzi wa masuala ya tenesi wanabashiri huenda Li Na akampiku gwiji wa Kimarekani Serena Williams kwenye viwango vya ubora wa mchezo wa Tenesi duniani, hasa ikichagizwa na namna ambavyo mwanadada huyo wa Kichina anavyoweza kumudu kucheza kwa juhudi kubwa katika michezo yake mingi ya hivi karibuni.

Michuano inayofuata ya Grand Slam ya French Open huenda ikawa na mvuto zaidi na Li Na anapewa nafasi kubwa ya kufika fainali.

Li Na ni mchezaji wa tenesi kutoka Uchina ambaye amekumbana na vikwazo vingi katika maisha yake ya uchezaji tenesi ikiwemo kujigharamia mwenyewe kwenye michuano mbalimbali tangu alipotoka kwenye timu ya taifa ya tenesi ya Uchina mwishoni mwa mwaka 2002 na kisha kurejea tena mwaka 2004.

Ni mchezaji wa tenesi mwenye shahada ya Uandishi wa Habari kutoka chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Huazhong nchini Uchina.