Marekani yaonya mashirika ya ndege

Haki miliki ya picha AP
Image caption Washiriki wa michezo ya Sochi

Serikali ya Marekani imeonya mashirika ya ndege yanayofanya safari za kwenda Urussi kwamba magaidi huenda wakajaribu kuingiza kimagendo vilipuzi vilivyofichwa ndani ya neli za dawa ya kusugua meno.

Afisa mmoja wa idara ya usalama nchini Marekani amesema vifaa kama hivyo huenda vikatumiwa kujenga bomu ndani ya ndege au baada ya kuwasili katika mashindano ya Olimpiki ya msimu wa baridi ambayo yataanza Ijumaa katika mji wa milimani wa Sochi.

Afisa huyo hata hivyo alisema kuwa serikali yake haina ushahidi wa tishio la moja kwa moja wa mashindano hayo ya Olimpiki ya Sochi .

Vikosi vya usalama vya Serikali ya Urussi viko katika hali ya tahadhari kuu baada ya makundi ya wanamgambo na magaidi kutishia kufanya mashambulizi katika mashindano ya Olimpiki ya msimu wa baridi ya Sochi.

Dagestan

Vikosi vya usalama katika jimbo la Dagestan nchini Urussi vimemuua kwa kumpiga risasi mwanamgambo wa kiislamu katika mji wa Izberbash.

Dzhamaldin Mirzayev mwenye umri wa miaka thelathini anashukiwa kuandaa mashambulizi ya bomu ya kujitoa mhanga katika mji wa Volgograd mwezi Disemba.

Watu thelathini na wanne waliwauwa katika shambulizi hilo.

Inadhaniwa kuwa Mirzayev ndiye aliyewapa mafunzo washambulizi wawili wa kujitoa mhanga .