Medali zaanza kunyakuliwa Olimpiki Sochi

Haki miliki ya picha REUTERS
Image caption Sage Kotsenburg akishangilia medali yake

Mwanariadha wa Marekani Sage Kotsenburg amekuwa mwanariadha wa kwanza kunyakua medali ya kwanza ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi inayofanyika katika mji wa Sochi nchini Urusi.

Sage Kotsenburg, amenyakua medali hiyo katika mchezo wa kuteteleza katika barafu kwa kwa kutumia ubao kwa upande wa wanaume, ukiwa ni mmoja katika michezo 12 mipya iliyoingizwa katika michuano hiyo, ili kuwavutia vijana.

Mwanamke wa kwanza kushinda medali ya dhahabu ni Marit Bjoergen wa Norway,katika mbio za marathon za kilomita 15. Umati mkubwa wa mashabiki wa Uholanzi wanatarajiwa kumshangilia bingwa mtetezi wa mchezo wa kuteleza katika barafu, Sven Kramer, akijaribu kutetea taji lake kwa upande wa wanaume mita elfu tano.

Rais Vladmir Putin wa Urusi alifungua rasmi jana(Ijumaa), mashindano ya Olimpiki ya majira ya baridi katika mji wa utalii wa Sochi katika sherehe zilizofana.

Waliokuwa wanariadha mashuhuri nchini Urusi waliubeba mwenge wa Olimpiki kabla ya kuwashwa na aliyekuwa mlinda lango wa mchezo wa magongo Vladislav Tretiak pamoja na mchoraji wa barafu Irina Rodnina.

Katika siku 16 zijazo,karibia wanariadha 3000 watashiriki katika michezo mbalimbali 98 katika mashindano hayo yaliodaiwa kugharimu takriban dola billioni 50.