Tuna maswali ya kujibu asema Wenger

Haki miliki ya picha d
Image caption Arsene Wenger

Kocha wa Arsenal, Arsena Wenger, amesisitiza kuwa ''The Gunners'' bado wana uwezo wa kushinda ligi kuu ya Premier msimu huu, lakini amekiri kipigo walichopata katika uwanja wa Anfeild, kimezua maswali kuhusu kikosi chake.

Kabla ya mechi ya Jumamosi Arsenal, ilikuwa katika nafasi ya kwa lakini hakuna aliyetarajiwa kuwa vijana hao wa Wenger watalimwa magoli matano kwa moja.

Wenger anakabiliwa na klibarua kigumu kubadili mtindo huo pale Arsenal itakapocheza na Manchester United siku ya Jumatano katika uwanja wa Emirates.

''Kipigo tulichopewa, kimezua maswali mengi ambayo tunastahili kuyajibu siku ya Jumatano usiku. Naamini bado tunauwezo wa kushinda ligi kuu kwa sababu ukipiga hesabu, inawezekana'' alisema Wenger.

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha dakika ishirini, Arsenal ilikuwa imelazwa magoli manne bila jibu.

Licha ya kurejea kwa mcheza kiungo wa Arsenal Jack Wilshere, ambaye alikuwa akiuguza jeraha, Arsenal haikuonyesha mchezo wake wa kawaida.

Martin Skrtel, Raheem Sterling na Daniel Sturridge ndio walioifungia Liverpool, huku Mikel Arteta akiipa Arsenal bao lake la kuvutia machozi.

Baada ya kuchuana na Manchester United siku ya Jumatano, Arsenal, itacheza tena na Liverpool katika raundi ya tano ya kuwania kombe la FA kabla ya kutoana jasho na miamba wa Ujerumani Bayern Munich katika mechi ya kuwania kombe la klabu bingwa barani Ulaya.