Botswana kumteua kocha mpya

Image caption Peter Butler

Botwana inatarajiwa kumteua Peter Butler kutoka Uingereza kuwa kocha wake mpya wa timu ya taifa ya soka.

Shirikisho la mchezo wa soka nchini Botswana, limesema kuwa litakuwa na habari muhimu siku ya Jumatano wakati wa kikao chake na waandishi wa habari mjini Gaborone

Inatarajiwa kuwa Butler mwenye umri wa miaka 47, atatangazwa kuwa kocha mpya naye Benny Kgomela akiteuliwa kuwa mkurugenzi wa masuala ya kiufundi.

Ripoti zinasema kuwa Butler, amesaini mkataba wa miaka miwili na shirikisho hilo, kuchukua mahala na Stanley Tshosane ambaye alifutwa kazi Oktoba mwaka uliopita.

Tshosane ndiye kocha wa kwanza kuwahi kuongoza timu ya taifa ya soka ya Botswana kufuzu kwa fainali za kuwania kombe la Mataifa Bingwa barani Afrika mwaka wa 2012, lakini alifutwa kazi baada ya timu hiyo kuandikisha matokeo mabaya mwaka uliopita.

Baada ya ya miezi minne ya uteuzi wa kocha mpya, shirikisho la soka nchini Botswana lilimchagua Butler, licha ya wengi kumpigia upato kocha mkuu wa timu ya taifa ta Uganda, Milutin Sredojevic.