Mgomo wa treni huenda ukatatiza ligi kuu

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Uwanja wa Fulham

Mechi ya ligi kuu ya Premier kati ya Fulham na Liverpool siku ya Jumatano, huenda ikahairishwa ikiwa mgomo wa wafanyakazi wa treni mjini London utaendelea kama ulivyopangwa.

Wafanyakazi hao wa treni wanatarajiwa kuanza mgomo wa saa 48 kuanzia leo, hali ambayo inaweza kutatiza shughuli za usafiri kama ilivyokuwa wiki iliyopita mjini humo.

Wasimamizi wa Fulham wana wasi wasi kuwa wafanyakazi wao huenda washindwe kufika kazini kwa muda unaofaa au hata kukoza kufika ili kuhakikisha kuwa mechi hiyo imeendelea.

Klabu hiyo inatarajiwa kutangaza baadaye hii leo ikiwa mechi hiyo itahairishwa au la.

Wamiliki wa klabu hiyo wamekuwa na mazungumzo na maafisa wa baraza la mji wa London pamoja na maafisa wa polisi na wamesema kuwa wana matumaini kuwa mechi hiyo itachezwa kama ilivyopangwa.

Huku hayo yakijiri, leo hii kutakuwa na mechi kadhaa za ligi kuu ya premier.

Cardif City itakuwa mwenyeji wa Aston Villa, Southampton kusafiri ugenini kucheza na Hull City.

West Ham itakuwa nyumbani kutoana jasho na Norwich, ili hali West Brom kualika vinara wa ligi hiyo kwa sasa Chelsea katika uwanja wao wa nyumbani.