Liverpool yaponea chupu chupu

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Daniel Sturridge akisherehekea bao lake

Steve Gerrard aliifungia Liverpool, kupitia mkwaju wa penalti dakika za mwisho mwisho na kuisaidia klabu yake kuilaza Fulham 3-2.

Bao la kujifunga la Kolo Toure, liliipa Fulham uongozi kabla ya Daniel Sturridge kusawazisha.

Lakini kadri mechi hiyo ilipoendelea Fulham, walionyesha mchezo mzuri na kuongeza bao la pili kupitia mchezaji Kieran Richardson baada ya mlinda lango wa Liverpool Martin Skrtel kufanya masihara, kwenye eneo la hatari.

Uongozi wa Fulham hata hivyo haukudumu kwa muda, pale Phillippe Coutinho kuisawazishia Liverpool.

Timu hizo mbili zilionekana kugawana alama moja kila mmoja lakini Liverpool, ilibahatika pale Sascha Riether alipomfanyia madhambi Daniel Sturridge katika muda wa ziada.

Nahodha wa Liverpool Steve Gerrard, bila ya kusita alitinga bao la tatu na kuifanya Liverpool kuwa alama nne tu nyuma ya vinara wa ligi hiyo kwa sasa Chelsea.

Ushindi huo ulikuwa wa tano wa Liverpool, mwaka huu na hii inamaanisha kuwa vijana hao wa Brendan Roggers wangali na nafasi ya kutwaa kombe hilo la ligi kuu mwaka huu na pia kudumisha rekodi ya kutoshindwa mechi yoyote mwaka huu.