Adebayor aendelea kung'aa Tottenham

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Adebayor akiwa na kocha wake baada ya kufunga bao

Emmanuel Adebayor kwa mara nyingine tena alifunga magoli mawili na kudumisha harakati za Tottenham za kusalia katika nafasi nne bora kwenye msururu wa ligi kuu ya Premier.

Tottenham waliilaza Necastle kwa magoli manne bila jibu.

Adebayor alifunga bao la kwanza kunako dakika ya kumi na tisa baada ya kipa wa Newcastle Tim Krul kutema mkwaju uliopigwa na Nabil Bentaleb.

Adebayor vile vile alichangia bao la pili wakati Krul kwa mara nyingine alipoutema mkwaju wake na kuumpa nafasi Paulinho kumalizia na kufunga la pili.

Nacer Chadli naye aliandikisha jina lake miongoni mwa wachezaji waliofunga goli mwaka huu pale alipofunga bao la tatu, baada ya kuvurumisha kombora kali kutoka umbali ya mita ishirini hivi.

Juhudi za Newcastle ziliambulia patupi pale kipa wa Spurs Hugo Lloris alipookoa mikwaju iliyopigwa na Papiss Cisse, Mathieu Debuchy na Yoan Gouffran.

Newcastle sasa haijafunga bao lolote katika mechi saba kati ya nane zilizopita na pia kuandikisha rekodi ya kupoteza mechi nne mfululizo katika uwanja wao wa nyumbani kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 1987.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Adebayor akiwa na kocha wake baada ya kufunga bao