Urusi watawala Olimpiki Sochi

Image caption Mashindano yakamilika Sochi

Makala ya 22 ya Michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi yalikamilika jumapili mjini Sochi Urusi baada ya siku 17 ya mashindano.

Mashindano hayo yaligharimu dola bilioni 30, ambayo ni kitita kikubwa zaidi katika historia ya mashindano ya Olimpiki duniani IOC.

Rais wa shirikisho la Olimpiki duniani (IOC) Thomas Bach aliirai dunia kuitizama Urusi kwa mtazamo mpya kwani wamezidisha matarajio ya washiriki wengi walioshiriki mashindano ya msimu wa baridi Sochi.

Alisema wanaondoka Sochi wakiwa marafiki bila ya kumbukumbu ya changamoto zilizokuwepo awali.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Sherehe za kufunga mashindano Sochi

Bach Alisema Urusi aliyoiona katika mashindano ya msimu wa baridi huko Sochi ni taifa jipya na karimu mno.

Zaidi ya wanariadha 2800 kutoka mataifa 88 walishiriki katika mashindano hayo yaliyojumuisha michezo 12 mpya .

Urusi ilimaliza ya kwanza katika jedwali la medali ,ikiwa na medali 13 za dhahabu 11 za fedha na 9 za shaba.

Norway ilimaliza ya pili na medali 11 za dhahabu 5 fedha na 10 za shaba.

Canada ilikamilisha orodha ya tatu bora na jumla ya medali 10 za dhahabu 10 za fedha na 5 za shaba.

Baada ya kuandalia dunia dhifa ya kukata na shoka waandalizi wa mashindano ya Sochi waliwakabidhi wenzao kutoka Korea kusini bendera ya kamati ya olimpiki .

Mji wa Pyeong-chang ulioko Korea Kusini ndio utakaokuwa mwenyeji wa mashindano yajayo ya olimpiki ya msimu wa baridi mwaka wa 2018.