Yanga yaichapa Ruvu shooting 7-0

Image caption Emmanuel Okwi ambae alisajiliwa toka sports club villa ya Uganda ni miongoni mwa walioiliza Ruvu shooting

Mabingwa watetezi Ligi kuu Tanzania Bara Yanga ya Dar es Salaam,imerejea kwa kishindo baada ya kuitandika Ruvu Shooting bao 7-0,katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Tafa jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo mkubwa ni wa pili katika Kipindi cha wiki mbili baada ya Kuilaza Timu ya Comorozine ya Comoro kwenye mechi ya awali kuwa ni klabu bingwa barani Afrika,hali inayoonyesha kuzidi kuimarika makali ya safu ya ushambuliaji ya Timu hiyo ambayo wiki ijayo ina kibarua kigumu itakaposhuka dimbani kuwakabili Mabingwa wa soka barani Afrika National Al Ahly ya Misri,kwenye mechi ya awali raundi ya kwanza kuwania Ubingwa wa Afrika.

Mechi hiyo ilishuhudia kurejea uwanjani kwa mshambuliaji Emmanuel Okwi ambaye usajili wake ulizua utata baada ya Yanga kumsajili toka Sports Club Villa ya Uganda,ambayo ilikuwa imeruhusiwa na FIFA huku kukiwa na kesi kadhaa kutoka klabu yake ya zamani Simba,na Etoile du sahel ya Tunisia.

Katika Mechi hiyo Okwi alitupia kambani bao la la tatu katika dakika ya 28, huku mengine yakitiwa kimiani na Mrisho Ngasa,Didier Kavumbagu,Hamis Kiiza,na Simon Msuva.

Bila shaka shaka hizo ni Salaam tosha kwa Mabingwa wa soka Barani Afrika National Al Ahly ya Misri wanaotaraji kuwasili wiki hii tayari kwa Pambano dhidi ya Yanga,litakalopigwa jijini Dar es Salaam,ambalo bila shaka litakuwa kali huku Yanga wakitamani sana kuuvunja mwiko wa kushindwa kuzifunga Timu kutoka Afrika kaskazini ambapo historia inaonyesha kuwa Yanga imekuwa ikifungwa mara kwa mara,hususan na timu kutoka Misri ambapo tangu mwaka 1982 Yanga haijawahi kuifunga timu yoyote ya Misri huku ikwa imefungwa bao 14-1 katika mechi tatu ilizocheza dhidi ya Al Ahly.

Katika Mechi nyingine iliyochezwa hapo jana Timu ya Mbeya City ililala bao 2-0 mbele ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.