Chui kanyeshewa kawa paka uwanjani Nyayo

Image caption Nembo ya AFC Leopards

Timu ya AFC Leopards ya Kenya imeondolewa kwenye mashindano ya kuwania kombe la shirikisho barani Afrika, baada ya kutoka sare ya kufungana magoli mawili kwa mawili na SuperSport ya Afrika Kusini, katika mechi ya raundi ya pili katika uwanja wa Nyayo mjini Nairobi.

Supersports sasa imefuzu kwa raundi ijayo kwa jumla ya magoli manne kwa mawili, baada ya kuilaza AFC Leopards magoli mawili bila jibu, katika awamu ya kwanza mjini Pretoria wikendi iliyopita.

Leopards ndio waliokuwa wa kwanza kufunga bao kunako dakika ya arubaini na nane, kupitia kwa mchezaji wake James Situma.

Image caption Wachezaji wa AFC Leopards baada ya kupata bao lao la kwanza

Dakika sita baadaye, vijana hao wa Afrika Kusini, walisawazisha kupitia Phala Thusa na dakika ya sabini na sita, Doutie Sameegh akaongeza la pili.

Huku matumaini ya AFC yakiwa yametumbukia nyongo, nahodha wake Allan Wanga alizawazisha kwa kichwa dakika za lala salama.

Leopards walimiliki asilimia kubwa ya mpira katika kipindi cha kwanza lakini hawakuweza kutumia vyema nafasi walizopata.

Kwa mwaka mwingine tena wawakilishi wa Kenya katika kinyanganyiro hicho cha kuwania kombe la Shirikisho barani Afrika wameyaaga mashindano hayo katika raundi ya kwanza.