Mwangangi ashinda dhahabu-Sopot

Image caption Caleb Mwangangi Ndiku

Mashindano ya Dunia ya riadha ya mbio za ndani yamemalizika mjini Sopot Nchini Poland, Kenya imejishindia medali moja ya dhahabu na nyingine ya fedha katika siku ya mwisho.

Bingwa wa zamani wa dunia wa mbio za mita 1,500, kwa wavulana chipukizi, Caleb Mwangangi Ndiku alinyakuwa medali ya dhahabu katika mita elfu tatu ili hali, Hellen Obiri, hakuweza kustahimili kasi ya mwanariadha wa Ethiopia Genzebe Dibaba kwani aliibuka wa pili na kujipatia medali ya fedha katika mbio hizo za mita elfu tatu kwa kina dada.

Matumaini yalikuwa makubwa katika siku ya tatu ya mashindano hayo, baada ya siku mbili za mwanzo ambazo Kenya haikujipatia medali yoyote.

Hata hivyo, Ndiku aliipa Kenya matumaini makubwa kwani alizima ndoto ya Mmarekani mwenye asili ya Kenya, Bernard Lagat kwa kuondoa jina lake katika historia ya Duinia kwa kuwa mwanariadha wa pili kunyakuwa mara nne taji la mashindano ya mbio hizo na kuwa sawa na gwiji Haile Gabrselassie wa Ethiopia.

Caleb Ndiku alimaliza mbio hizo kwa dakika saba, sekunde 54 nukta 94, na kumpiku mbingwa mara tatu Lagat wa Marekani, aliyenyakuwa fedha kwa dakika 7, sekunde 55 nukta 22.

Haki miliki ya picha i
Image caption Caleb Mwangangi Ndiku

Muethiopia Dejen Gebremeskel alinyakuwa shaba kwa kutimka dakika 7 sekunde 55 nukta 39.

Bingwa wa zamani wa mbio za Jumuia ya madola mita elfu 5, Augustine Kiprono Choge, alisukumwa hadi nafasi ya 9 kwa kutumia dakika 7 sekunde 57 nukta 46. U

shindi huo hatimaye uliiweka kenya katika nafasi ya saba kwa wingi wa medali hadi tukienda mitamboni.

Katika upande wa kina dada mita elfu 3, itabidi Mkenya Hellen Obiri kujaribu wakati mwingine, baada ya makali yake kudumazwa na Genzebe Dibaba.

Bingwa huyo wa zamani wa medali ya shaba mita 1,500 alijaribu kumkabili raia wa Bahrain Maryam Yusuf Jamal ili asinyakuwe medali ya fedha, jambo lililomfanya kumaliza katika nafasi ya pili.

Dibaba alitumia dakika 8 sekunde 55 nukta 04 na kuinyakulia Ethiopia dhahabu yake ya pili katika mashindano hayo, huku Obiri akitumia dakika 8 sekunde 57 nukta 72.

Mkenya mwingine Irene Jelagat, alimaliza wa nne kwa kutumia dakika 9 sekunde 57 nukta 72