Pardew apigwa marufuku na FA

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Allan Pardew

Kocha wa Newcastle, Allan Pardew, amepigwa marufuku ya kutoshiriki katika mechi saba, baada ya kupatikana na hatia ya kumpiga kwa kichwa mchezaji wa Hull City, David Meyler.

Adhabu hiyo ndio kali zaidi kuwahi kutolewa kwa kocha yeyote katika historia ya ligi kuu ya Premier.

Pardew alizozana na mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Jamuhuri ya Ireland, kunako dakika ya sabini na mbili wakati timu yake iliposhinda Hull City kwa magoli manne kwa moja tarehe moja mwezi huu.

Kwa mujibu wa tume huru ya shirikisho la mchezo wa soka nchini England, FA, Pardew hataruhusiwa kuingia uwanjani wakati wa mechi za kwanza tatu mfululizo kabla ya kumaliza adhabu hiyo akiwa amesalia katika eneo lililotengewa makocha uwanjani.

Kocha huyo pia alipigwa faini ya pauni elfu sitini pesa za Uingereza na kuonywa kuwa atachukuliwa hatua kali zaidi ikiwa tabia yake itakuwa ya kuzua mashaka siku zijazo.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa kocha yeyote wa ligi kuu ya Premier kupigwa marufuku ya kutoingia uwanjani kabisa.

Kocha huyo amesema kuwa atakubali adhabu hiyo na kukariri kuwa dhamira yake kuu sasa ni kuandaa kikosi chake kwa mechi za wikendi hii.

Baada ya tukio hilo Pardew alipigwa fainali ya pauni elfu mia moja na klabu yake na kupewa onyo kirasmi na wasimamizi wa klabu hiyo.