Chelsea yaiadhibu Arsenal 6-0.

chelsea Haki miliki ya picha Getty
Image caption Oscar, Torres na Schürrle wakishangilia goli la sita.

Mechi ya 1000 kwa kocha wa Arsenal,Arsene Wenger iligeuka majonzi na kufuta sherehe za kutimiza mechi ya elfu moja kwa mfaransa huyo baada ya timu yake kukubali kipigo cha 6-0 kutoka kwa Chelsea.

Arsenal walioanza mechi ya leo kwa kuonyesha dalili za mapema za kufungwa, waliruhusu mabao mawili ndani ya dakika nane za kipindi cha kwanza.

Samwel Eto'o alianza kwa kuifungia bao nzuri Chelsea dakika ya tano ya mchezo kabla ya mjerumani Andre Schurrle hajafunga bao la pili kwa mkwaju mrefu uliomshinda kipa wa Arsenal.

Penati ya Eden Hazard baada ya Alex Oxlade-Chamberlain kuushika mpira iliazaa bao la tatu, licha utata ulioibuka kwa mwamuzi Andre Marriner ambaye alionekana kuchanganyikiwa au kutokujua ni nani aliyefanya kosa la kuushika mpira na badala yake alimpa kadi nyekundu Kieran Gibbs ambaye hakufanya kosa hilo.

Oscar alihitimisha kipindi cha kwanza kwa bao la nne kwa Chelsea kabla ya Mohamed Salah kuingia kipindi cha pili na kuipa Chelsea bao la tano na kisha Oscar kufunga mahesabu kwa bao la sita.

Arsenal walijitahidi kufanya mabadiliko ya wachezaji kipindi cha pili na kujaribu nafasi kadhaa walizotengeneza lakini ni wazi bahati haikuwa kwao na hadi mchezo unamalizika matokeo kwenye uwanja wa Stamford Bridge magharibi mwa jiji la London, Chelsea 6-0 Arsenal.

Kiujumla Arsenal hawakuwa katika kiwango chao ambacho wengi walizoea kuiona, ila wachambuzi wa soka hapa Uingereza wanasema mbinu za kocha Arsene Wenger anapokutana na mechi kubwa huwa hazifanyi kazi, kwani imekuwa ikiruhusu magoli mengi katika mechi kubwa wanazocheza.

Mechi inayofuata, Arsenal watakutana na Swansea kisha wikiendi ijayo watawakaribisha Manchester City.