Arsenal yatoshana nguvu na Man City

Image caption Mathieu Flamini (kulia)akishangilia bao la kusawazisha dhidi ya Man City akiwa na Olivier Giroud(kushoto)

Manchester City imekosa nafasi ya kurejea kileleni mwa ligi kuu ya Premier ya England baada ya kulazimishwa sare na Arsenal kwenye uwanja wa Emirates.

City walikuwa wakiongoza kwa bao moja lililopatikana kipindi cha kwanza dakika ya 18 kupitia kwa David Silva, walishindwa kuhimili vishindo vya The Gunners hasa kipindi cha pili.

Arsenal walisawazisha kupitia kwa Mathieu Flamini kipindi cha pili dakika ya 53 ya mchezo baada ya kumalizia pasi nzuri ya Lukas Podolski.

Kikosi cha Arsene Wenger kilionyesha uhai mkubwa katika mchezo huo mbele ya mashabiki wa nyumbani ambao walikuwa wakiishangilia kwa nguvu timu yao baada ya kuwa na majonzi tangu mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kazi kubwa ilifanywa katika eneo la katikati mwa uwanja ambako, kasi na pasi za mwisho zilizoeleka kutoka kwa Yaya Toure mchezaji bora wa BBC kutoka Afrika hazikuonekana katika mchezo huo.

Manchester City walitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini kukosa umakini au bahati katika mchezo wa leo ziliwafanya wapumue kwa tabu hasa kipindi cha pili kwani Arsenal walionekana kuwa na nguvu,kasi na umakini mkubwa kuonyesha matumaini yao yangalipo ya kuuchukua ubingwa wa ligi kuu msimu huu.

Kwa matokeo haya, Chelsea wanasalia kileleni mwa ligi wakiwa na pointi moja zaidi ya Liverpool ambao wapo nafasi ya pili na Manchester City wakishika nafasi ya tatu na Arsenal wakiwa kwenye nafasi ya nne.

Liverpool huenda wakawa vinara wa ligi hapo jumapili jioni iwapo watashinda mchezo wao dhidi ya Tottenham Hotspurs.