Ryan Giggs aanza vizuri ManU

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ryan Giggs kaimu meneja wa Manchester United

Meneja wa Manchester United Ryan Giggs ameanza kutumikia nafasi hiyo kwa furaha baada ya kikosi chake kuibuka na ushindi wa magoli 4-0 dhidi ya Norwich City katika mchezo uliofanyika uwanja wa Old Trafford.

Magoli ya Manchester United yalipachikwa na Wayne Rooney kwa njia ya penalti dakika ya 41 kipindi cha kwanza cha mchezo, huku akipachika tena dakika ya 48. Mabao mengine mawili yaliwekwa kimiani na Juan Mata katika dakika ya 63 na 73.

Giggs, ambaye anashikilia nafasi hiyo kwa muda baada ya David Moyes, kutupiwa virago vyake kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo ambayo kwa sasa inashikilia nafasi ya saba na kupoteza kabisa matumaini ya kutwaa ubingwa na kuwa mashakani iwapo Manchester United itapata hata nafasi ya nne bora ya ligi kuu ya England.

Giggs mwenye umri wa miaka 40 amehidi kurejesha heshima ya Manchester United katika mfumo wa uchezaji, mapenzi na timu hiyo, ushupavu katika kupambana na timu pinzani na kuwa wabunifu wakiwa uwanjani kuwa mambo ya msingi kwa klabu hiyo kongwe.

Mara baada ya kujitokeza katika mechi hiyo, Giggs alipokelewa kwa nderemo na shangwe kutoka kwa mashabiki wa Manchester United. Giggs ameichezea wakati wote Manchester United akiwa amecheza michezo 962 na kusema maisha yake yamejengwa katika mwamba huu, Manchester United.

Manchester United iko katika nafasi ya saba kwa kujikusanyia pointi 60 baada ya michezo 35.