Waziri wa Afrika Kusini awakera wakenya

Image caption Waziri wa michezo wa Afrika Kusini Fikile Mbalula

Waziri wa michezo nchini Afrika Kusini, Fikile Mbalula amekemewa kwenye mitandao ya kijamii nchini Kenya kwa matamshi yake kuhusu wanariadha wa Kenya.

Waziri huyo inaarifiwa alitoa matamshi yake katika mkutano na wandishi wa habari mjini Johannesburg alipokuwa anazungumzia swala la utangamano katika jamii.

Aliyatoa matamshi yake ambayo wakenya wameyaona kama ya madharau, alipoulizwa na mwandishi mmoja kwa nini timu za kitaifa za michezo nchini Afrika Kusini bado zina wachezaji wengi waafrika wazungu, licha ya kumalizika kwa utawala wa kibaguzi zaidi ya miaka 20 iliyopita

"huwezi kuleta mageuzi katika michezo bila malengo,'' alinukuliwa na jarida la Mail and Guradian akijibu swali hilo kuhusu swala tete la ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

"lakini Afrika Kusini haiwezi kuwa kama Kenya na kutuma wanariadha wake katika michezo ya Olimpiki wakazame kwenye vidimbwi vya kuogelea,'' aliongeza waziri huyo.

Kulingana na jarida la Mail & Guardian, matamshi ya waziri huyo yaliwashangaza wengi waliokuwa wamehudhuria mkutano huo baadhi hata wakigeuka kwa aibu.

Hakuna mkenya yeyote aliyewahi kuzama katika kidimbwi katika michezo ya Olimpiki.

Wakenya wajitokeza kwenye mitandao ya kijamii na kuanza kumjibu waziri huyo baadhi wakisema kuwa hayo yalikuwa matusi kwa wakenya.

Baadhi walihisi kama waziri huyo alikuwa anadharau wanariadha wakenya ambao wameiletea nchi yao sifa kedekede katika riadha kimataifa.