Baltacha: Mchezaji wa Uingereza afariki

Haki miliki ya picha .
Image caption Marehemu Elina Baltacha

Mchezaji wa zamani wa tennis nambari moja wa Uingereza Elena Baltacha amefariki dunia kwa ugonjwa wa saratani ya ini akiwa na umri wa miaka 30.

Alizaliwa Ukraine na kukulia Scotland, mwezi Machi mwaka huu, Baltacha alifichua kuwa alikuwa anaumwa.

Baltacha, alikuwa Mwingereza namba moja kwa ubora katika tennis nchini humo kwa karibu miaka mitatu, na alijiuzulu mchezo huo Novemba 2013.

Baltacha alitambua kuwa alikuwa na tatizo la saratani ya ini katikati ya mwezi Januari 2014, miezi miwili baada ya kujiuzulu mchezo wa kulipwa wa tennis na wiki chache baada ya kuolewa.

Wachezaji wa World Tour watakusanyika na kusimama kimya kwa dakika moja katika uwanja wa katikati ya viwanja vya Madrid Masters baadaye.

"Alikuwa mtu wa kustajaabisha na aliwagusa watu wengi kwa moyo wake wa upendo, kwa uchangamfu na huruma yake," amesema mume wake Severino.

Licha ya kupata matatizo ya kuumia na kugundulika katika umri mdogo wa miaka 19 kuwa na dalili za ugonjwa wa saratani, Baltacha alifika mbali kuingia mzunguko wa tatu katika mashindano ya wazi ya Austarlia, Australian Open, mwaka 2005 na 2010 na alifikia daraja la juu la mchezo wa tennis kwa kushika nafasi ya 49 kwa ubora.

Aliwahi kushinda mataji 11 ya mchezaji mmoja mmoja, alifika mzunguko wa tatu wa michezo ya Wimbledon mwaka 2002 na kuwa miongoni mwa wachezaji wa timu ya Uingereza kwa miaka 11.

Wachezaji wenzake mbalimbali wamekuwa wakituma salamu za pole kwa familia ya Baltacha, akiwemo mchezaji wa sasa nambari moja wa kike wa mchezo wa tennis nchini Uingereza, Laura Robson.