Man U yatandika Hull City Mabao 3 kwa 1

Manchester United katika mechi yake jana usiku ilijivunia nguvu mpya za kijana James Wilson aliyefunga mabao mawili dhidi ya Hull City na kuchangamsha mashabiki wa timu hiyo iliyozorota sana msimu huu.

Ilikuwa mchanganyiko pia na nguvu za vigogo meneja Ryan Giggs mwenye umri wa miaka 40 aliyejitosa uwanjani katika kipindi cha pili kuipa timu yake msukumo na uongozi akiwa uwanjani.

Licha ya ushindi walioupata wa mabao matatu kwa moja wamebaki papo hapo nambari 7.

Giggs hata hivyo aliwaambia hicho ni kionjo tu kwamba ana matumaini makubwa nyakati nzuri za ushindi na vishindo vya zamani vilivyoleta fuhara na buhara zitairudia tena Man U.

Na leo usiku twasubiri kuiona Man city ambao tayari wana mkono moja kwenye kikombe hicho cha ligi, iwapo wataidhiti Aston Villa isitilie doa kikao chao cha hapo kileleni!

Mechi za lala salama ni zile za Jumapili.

Katika ligi ya Uganda ambayo imemalizika jana, ilishirikisha timu 16, Timu ya KCC ya Uganda ilihifadhi taji lake kwa kuwashinda wapinzani wao wa jadi Sports Club Villa mabao 3 kwa moja katika mechi ya jana hapo KCC Lugogo mjini Kampala.

KCC wamemaliza na pointi sitini huku wapinzani wake wa karibu timu ya chuo kikuu cha Victoria wakimaliza katika nafasi ya pili na alama 59.

Hili ni taji la KCC la mara ya 10 tangu kuanza ligi hiyo hapo 1966.

Timu iliyonyakua taji hilo mara nyingi zaidi ni Sports Club Villa ambayo imetwaa kombe hilo mara 15. Ligi ya soka ya msimu huu ilikosa udhamini baada ya kuwa na mvutano wa ligi mbili za soka.

Ni matarajio ya wengi kuwa mwaka kesho wadhamini watarudi , hii ni baada ya pande hizo mbili kusikilizana.