"Ndoo "ya EPL, ManCity au Liverpool?

Image caption Wachezaji wa Manchester City wakishangilia moja ya ushindi wao katika ligi kuu ya England

Msimu wa 2013-14 ligi kuu ya England unafikia ukingoni Jumapili kwa timu zote 20 za ligi hiyo kujitupa katika viwanja mbalimbali nchini humo, huku Manchester City wakiwa ndio watarajiwa wakuu wa kubeba kombe hilo kutokana na kuwa kileleni ikiwa na pointi 83, na wingi wa magoli ya kufunga ikinyemelewa kwa karibu na Liverpool yenye pointi 81.

Man City wanapewa nafasi kubwa ya kulitwaa kombe la EPL kwa mara ya pili katika miaka mitatu baada ya Jumatano kuishushia kipigo kizito Aston Villa ilipoicharaza 4-0 na kupaa kwa pointi mbili zaidi ya Liverpool, timu zote zikibakiwa na mchezo mmoja.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Kikosi cha Liverpool wakijipanga kuanza mchezo katika uwanja wao wa Anfield

Ushindi huo uliifanya Chelsea kupoteza ndoto ya ubingwa kwani hata ikishinda Jumapili dhidi ya Cardiff iliyoshuka daraja itafikisha pointi 82 tu ambazo tayari zimevukwa na Manchester City. Kwa sasa itakuwa ikipigania nafasi ya pili iwapo Liverpool yenye pointi 81 itateleza na yenyewe ishinde mchezo wake. Matokeo haya yanawapa nguvu zaidi vijana wa Manuel Pellegrini, ambao wanahitaji pointi moja tu kutwaa "NDOO" hiyo watakapoikaribisha West Ham katika uwanja wake wa Etihad. Kama Man City itatoka sare itakuwa na pointi 84 sawa na Liverpool inayocheza na Newcastle iwapoa itashinda. Hata hivyo wingi wa magoli 13 zaidi ya Liverpool aliyonayo Manchester City ndio unaofanya wapenzi wa kandanda duniani kuamini kuwa City ubingwa unawanukia. Lakini Liverpool ikishinda na Mancity wakashindwa basi, Liverpool wataibuka mabingwa wapya baada ya kusubiri kwa zaidi ya miaka 24, jambo ambalo vijana wa Pellegrini hawatakubali liwatokee.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wachezaji wa Chelsea wakishangilia goli

Liverpool walionekana kulitwaa kombe hilo, hadi pale waliponyamazishwa na Chelsea tarehe 27 Aprili 2014 walipotwangwa magoli 2-0 katika uwanja wao wa nyumbani Anfield. Lakini jahazi lilianza kuchota maji pale walipokubali kutoka sare ya mabao 3-3 na Crystal Palace, licha ya Liverpool kuongoza kwa mabao 3-0 kwa kipindi kirefu katika mchezo wao wa Jumatatu katika uwanja wa Selhurst Park.

Wakati huo huo Manchester City, Liverpool, Chelsea na Arsenal zina uhakika wa kumaliza ligi hiyo zikiwa katika nne bora na hivyo kuwa wawakilishi wa England katika michuano ya mabingwa barani Ulaya, UEFAmsimu ujao.

Everton tayari imefuzu kucheza michuano ya ligi ya Europa League pamoja na Hull City iliyofika fainali za kombe la FA.

Mabingwa watetezi, Manchester United msimu huo haukuwa mzuri kwao kwani wameshindwa kufurukuta hata kuingia nne bora ikiwa katika nafasi ya saba na pointi 63 kabla ya mchezo wa mwisho dhidi ya Southampton iliyo katika nafasi ya nane.

Macho na masikio ya mashabiki wa soka duniani, hususan wa ligi kuu ya England yatakuwa katika michezo miwili tu. Manchester City dhidi ta West Ham na Liverpool dhidi ya Newcastle.