Origi:'Kwa nini naichezea Ubelgiji'

Image caption Divorc Origi ni mkenya na mwanaafrika mashariki wa kwanza kushiriki kombe la dunia

Mshambuliaji wa Lille ya Ufaransa , Mkenya Divorc Origi ambaye ni mzaliwa wa Ubelgiji ni miongoni mwa wachezaji wa timu ya taifa ambayo imeondoka Jumanne kuelekea Brazil kwa mashindano ya kombe la dunia kuanzia Alhamisi wiki hii.

Origi, mwanae Mike Okoth, mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars atakua mchezaji wa kwanza wa Afrika Mashariki kuiwakilisha Ubelgiji, na yuko pamoja na wachezaji nyota kama vile Vincent Kompany wa Manchester City na Eden Hazard wa Chelsea.

Watakabiliana na Algeria mechi yao ya kwanza ya kundi H Juni tarehe 17 na siku tano baadae wanapepetana na Urusi kisha Korea Kusini kwenye mechi za mchujo.

Akizungumza na BBC kwa njia ya simu akiwa Ubelgiji Origi anasema:'' Algeria ni timu yenye wachezaji wazuri kwa hivyo hatuwezi kuidharau. Tutacheza mchezo wetu wa kawaida lakini nina matumaini makubwa tutashinda.’’ Anasema Urusi na Korea pia si timu hafifu hasa Warusi. Lengo lake kubwa ni Ubelgiji kufuzu kwa raundi ya pili kisha kutoka hapo anasema mambo yatakuwa sawa kabisa.

Kuhusu mbona ameamua kuiwakilisha Ubelgiji na sio taifa la babake Kenya, Origi anasema alitilia maanani mambo mengi kama vile usimamizi mzuri wa kandanda nchini humo, mizizi yake ya kandanda iliyoko huko, marafiki, ushauri wa babake pamoja na Ubelgiji kufuzu kwa kombe la dunia kwani haijulikani ni mwaka upi Kenya itafuzu kwa kombe la dunia.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Moja ya viwanja vitakavyotumika kwa michuano ya kombe la dunia Brazil

Tukiwa tunazungumzia hilo babake Origi, Mike Okoth, naye anajitupa uwanjani kwa kusema:''Mimi nilimshauri aichezee Ubelgiji na sio Kenya kwa sababu kusema kweli kama angechezea Harambee Stars kuna mambo ambayo hangestahimili hasa usimamizi mbovu. Mimi nilivumilia kwa saababu nimezaliwa Kenya lakini mwanangu hangeweza kabisa. Na tena bado ni mchanga kwa hivyo ni vyema aiwakilishe Belgium. Nakumbuka siku moja tukiwa na Harambee Stars tulilala kwenye jumba moja ambalo bado lilikua linajengwa huko Afrika Magharibi.’’

Namuuliza Okoth kama kuna siku Harambee Stars itafuzu kwa kombe la dunia? ''Itakua vigumu sana kwao kufuzu kwa kombe la dunia kama usimamizi ni duni bado,’’ anasema Okoth, na kuongezea:''Tena wanahitaji wawe wakicheza na timu mashuhuri duniani mara kwa mara. Sio kwamba ni vigumu kufuzu lakini lazima pia serikali nayo ikubali kutumia fedha kulipia mechi kubwa za kimataifa na tuwe na msingi mzuri wa kandanda kuanzia mashinani.’’

Origi, mwenye umri wa miaka 19, anasema amefurahia sana kuchaguliwa kuiwakilisha Ubelgiji kwenye kombe la dunia, na vile vile kuwa na mshambuliaji mahiri Romelu Lukaku wa Chelsea ambaye msimu uliopita alichezea Everton kwa mkopo.

Image caption Mpira wa kombe la dunia Brazil

''Wachezaji wote wananipa morali sana. Rafiki yangu Hazard (Eden) na Kompany (Vincent) wameniambia nicheze mchezo wangu wa kawaida nisiwe na wasiwasi uwanjani,’’ asema Origi aliyecheza mechi ya mwisho ya kirafiki dhidi ya Tunisia ambayo Ubelgiji ilishinda kwa bao 1-0. Namuuliza kama ananuia kuhamia England lakini Origi anasema kwa sasa mawazo yake yote yako Brazil kwa kombe la dunia. Babake Origi ni shabiki mkubwa wa Liverpool.

Mara ya mwisho Ubelgiji kushiriki kombe la dunia ni mwaka wa 2002 ambapo kocha wao wa sasa Marc Wilmots alikuwa mchezaji wa mwisho kuifungia Ubelgiji kwenye kombe la dunia hadi sasa. Wilmots ana imani na Origi ambaye amechukua nafasi ya Christian Benteke wa Aston Villa anayeuguza jeraha.

Urusi ndio tisho kubwa kwa Ubelgiji kumaliza katika nafasi ya kwanza kundi H, na ina motisha wa kufanya vyema kwani wao ndio wataanda kombe la dunia mwaka wa 2018. Isitoshe Urusi inafunzwa na kocha anayeaminika kulipwa mashahara wa juu zaidi duniani Fabio Capello ambaye anaweka kibindoni dola millioni 6.5 kwa mwaka. Matokeo mazuri zaidi kwa Urusi kwenye kombe la dunia ni mwaka wa 1966 walipomaliza wa nne.