Mgomo waahirishwa kwa mashauriano Brazil

Haki miliki ya picha AP
Image caption Kituo cha treni kilichofungwa mjini Sao Paulo kutokana na mgomo.

Angalau afueni sasa imepatikana baada ya wafanyikazi wa usafiri wa reli ya mjini Sao Paulo, Brazil kuhairisha kwa siku mbili mgomo wao wa kudai nyongeza ya mishahara ili kutoa fursa ya mazungumzo.

Hata hivyo wametishia kugoma tena alhamisi siku ya ufunguzi wa kombe la dunia iwapo wenzao 60 wanaokabiliwa na tisho la kufutwa kazi hawatarudishwa kazini.

Serikali haijaafiki nyongeza ya 12% wanayodai wafanyikazi hao, wala kuwarudisha kazini wafanyikazi waliosimamishwa.

Nyongeza ya asilimia 8.8% waliokubali kutoa serikali imekataliwa na wafanyikazi hao.

Mfumo huo wa usafiri wa reli ya mjini uitwao 'Metro' umekumbwa na mgono wa tangu alhamisi iliyopita.

Na wafanyikazi na polisi wamekabilina huku polisi wakirusha vilipua machozi na kusababisha ghasia siku mbili tu kabla kombe hilo kuanza.

Kinyume na matarajio kombe hilo la dunia limewagawanya raia wa nchi hiyo kiasi cha kuushangaza ulimwengu unaoitambua Brazil kama gwiji wa soka.

Kuna wale wanaoghadhabishwa kwamba migomo hiyo inaharibu si tu sifa hizo za Brazil bali pia kuwaongezea kero la foleni na msongamano unaovuruga ratiba zao mijini ,lakini wengine wamechukulia fursa hiyo ya kombe la dunia kutetetea maslahi yao kama kudai nyongeza ya mishahara na huduma nyenginezo za kijamii kutoka kwa serikali.

Rais wa nchi hiyo Bi Dilma Rousseff amesema kamwe hataruhusu maandamano ya ghasia kuvuruga tamasha hilo la kombe la dunia.