Blatter Ataka muhula wa 5 urais Fifa

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Blatter adokeza nia yake kutaka urais wa Fifa kwa muhula wa 5.

Rais wa shirikisho la kanda FIFA, Sepp Blatter, amesema yuko tayari kuendelea na wadhfa huo kwa muhula mwengine wa 5.

Akizungumza katika kikao maalum cha Fifa huko Sao Paulo amesema yuko tayari kugombea tena cheo hicho kama rais wa shirikisho hilo kubwa linalosimamia soka ya dunia.

Kwa kutangaza hivyo ni kwamba amepuuzilia mbali kauli za maafisa wa soka wa Europa wanaomtaka ajiuzulu kufuatia madai ya rushwa yanayoiandama Fifa,wakati ilipochaguliwa Qatar kuwa mwenyeji wa kombe la dunia 2022.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Europa imemtaka Blatter ajiuzulu kufuatia tuhuma za rushwa katika Fifa.

Awali Blatter mwenye umri wa miaka 78 alikuwa amedokeza kuwa angestaafu baada ya kipindi chake cha sasa.

Blatter pia amependekeza kuwa mameneja wa timu waruhusiwe kutafuta haki pale kwa kutumia technologia pale watakapohisi maamuzi ya refa hayakuwa sawa.

Tisho la Maandamano

Wakati huo huo watu 10 wameripotiwa kukamatwa na kupelekwa vituo vya polisi huko Rio de Janeiro ili kuhojiwa kuhusiana na kushiriki kwao katika maandamano yenye ghasia.

Ulinzi unaendelea kuimarishwa hasa katika miji ya Sao Paulo na Rio ambako baadhi ya makundi ya watu wametishia kufanya maandamano kudai maslahi yao, wakati wa ufunguzi wa kombe la dunia utakaofanyika chini ya saa 24.