Michael Schumacher apata fahamu

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Schumacher alikuwa anashiriki mchezo wa kuteleza kwa barafu alipoanguka na kuumia vibaya

Mwanaspoti anayefahamika katika mashindano ya uendeshaji wa magari ya langalanga au F1 Michael Schumacher amepata fahamu.

Michael Schumacher alitoka hospitalini Grenoble na ataendelea kuishi kwa hali yake ya kawaida,familia yake ilisema.

Michael Schumacher alikuwa akiteleza kwenye theluji kwa skii wakati ajali hiyo ilipotokea.

Schumacher alilazimika kudungwa sindano ya kupoteza fahamu baada ya kupata majeraha mabaya kichwani huko French Alps tarehe 29 Disemba.

Madaktari walichukua hatua hiyo ili kusaidia ubongo uliovimba wa mshindi huyo wa mara saba kunywea.

Familia yake iliendelea kwa kushukuru wote waliomtumia jumbe za kumtakia afueni ya haraka kwa kusema zilimtia moyo,pia waliwashukuru madaktari waliomhudumia alikolazwa katika hospitali ya Grenoble,kusini -mashariki mwa ufaransa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Schumacher alistaafu kutoka kwa mashindano ya Langalanga mwaka 2012

“Michael ametoka hospitalini CHU Grenoble, kuanza safari ndefu ya kurudi katika hali yake ya kawaida. Amepata fahamu,'' Sabine Kehm ambaye ndiye meneja wake alisema katika taaarifa iliyotolewa kwa niaba ya familia yake.

Hapo awali familia yake ilikuwa imeonya kuwa toka mwanzoni itakuwa hali ngumu sana kwa Michael.

Wapelelezi katika ajali hiyo wanasema Schumacher alikuwa kwa mwendo wa kasi kama mwenye uzoefu wa mchezo huo wakati wa ajali hiyo Meribel

Alikuwa akiteleza kwenye theluji alipoanguka na kugonga mwamba.

Schumacher alistaafu kutoka mchezo wa F1 mwaka wa 2012 baada ya kuwa kwa safu hiyo kwa miaka 19.

Alishinda taji mbili na Benetton, mnamo mwaka 1994 na 1995, kabla kuelekea Ferrari 1996 na kupendekeza kupata mataji tano kuanzia 2000.