Kipa wa Mexico ainyima Brazil ushindi

Haki miliki ya picha AP
Image caption Ochoa aliokoa mikwaju tele ya Brazil

Mexico walipata pointi moja dhidi ya Brazili, katika mechi ya kundi A iliyomalizika bila ya timu yeyote kutisa wavu wa mwenziye katika uwanja wa Estadio Castelao huko Fortaleza.

Brazil walishindwa kufunga bao na ilikua sio kama timu ile iliyoishinda Croatia mabao 3-1 matika mechi ya ufunguzi .

Hata hivyo Brazil inamlaumu Kipa wa Mexico Francisco Ochoa, aliyefanya kazi ya ziada katika mechi hiyo kuhakikisha vijana wa Luiz Felipe Scolari hawajizolei alama zote tatu.

Brazili walimiliki asilimia kubwa ya mchezo hata ingawa hawakuitumia kwa manufaa yao.

Fred alipatikana kuotea kwenye lango mara tatu mfululizo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Licha ya Mashambulizi ya Neymar ,kipa wa mexico Ochoa alihakikisha mechi hiyo inaisha sare tasa.

Mshambulizi wa Mexico, Oribe Peralta alijaribu ngome ya Brazili lakini Thiago Silva na Marcelo walimzuia.

Ochoa tena aliokoa jaribio lingine la Neymar katika kinyang’anyiro katika lango la Mexico.

Jaribio lingine la Jo lilizuiwa na Ochoa; kipa wa Mexico.

Kisha mpira wake Silva, kwa kichwa, kutoka kwa kona yake Neymar, ukasimamishwa tena na Ochoa katika dakika ya 85.

Wito wa Brazili wapewe penalti Marcelo alipoanguka kwa urahisi mbele ya lango la Mexico uliambulia patupu.

Mexico kwa upande wao hawakuwa na nafasi nyingi, ila wakati ule Hector Herrera alipiga mkwaju uliopita kidogo juu ya lango la Brazil.

Matokeo haya yanaziwacha timu zote mbili zikiwa na alama nne katika kundi lao, zikiwa zimesalia na mchuano mmoja kucheza.