Colombia itachuana na Uruguay

Haki miliki ya picha All Sport
Image caption Colombia yaidhibu vikali Japan

Colombia ilikamilisha mechi zake za makundi kwa kishindo ilipoicharaza japan mabao manne kwa moja na kusalia kileleni mwa kundi C na alama zote 9

Timu hiyo ambayo ilikuwa imekwisha fuzu kwa kushiriki katika mechi za timu 16 bora haikulegeza kamba kufuatia mori ya Japan kusajili ushindi dhidi yao..

Japan ilihitaji ushindi ili kuweza kwendelea kushiriki kombe hili la dunia lakini Juan Cuadrado aliifungia Colombia kupitia mkwaju wa penalty baada ya Adrian Ramos kuchezewa visivyo na Yasuyuki Konno mbele ya lango na akaiweka Colombia kifua mbele .

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Colombia yaidhibu vikali Japan

Muda mfupi tu kabla ya kukamilika kwa kipindi cha kwanza, mshambulizi wa Mainz Shinji Okazaki alifufua matumaini ya Japan kwa kufunga bao kwa kichwa.

Bao hili liliwatamausha Colombia ambao sasa walikaza buti na kufunga mabao matatu bila ya jibu ungedhani wanatafuta tiketi ya kufuzu kwa mkondo ujao.

Jackson Matinez alirejesha uongozi wa Colombia kabla ya kuongeza bao la tatu kwa Colombia dakika ya 82.

James Rodriguez alihakikisha Colombia imejizolea alama zote tatu katika mechi za makundi na kuwa taifa la pili kufanya hivyo baada ya Uholanzi, kwa kufunga bao la nne mnamo dakika ya 89.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Colombia yaidhibu vikali Japan

Colombia itachuana na mshindi wa pili wa kundi D ambaye ni Uruguay baada ya timu hiyo ya Luiz Suarez kuifungisha virago mabingwa mara nne wa kombe la dunia Italia ilipoilaza 1-0.

Ugiriki ilifuzu kama mshindi wa pili katika kundi C na hivyo sasa itakwaruzana na washindi wa kundi D Costa Rica .

Kutokana na kichapo hicho Italia iliungana na Uingereza kama timu zilizobanduliwa nje baada ya mkondo wa kwanza .

Aidha Afrika kufikia sasa haina mwakilishi katika mkondo wa pili wa kombe la dunia .