Italia nje ya kombe la dunia

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Italia nje ya kombe la dunia .

Uruguay ilifunga bao la ushindi katika dakika za mwisho na kuwabandua washindi mara nne wa kombe la dunia Italia .

Hata hivyo habari kuu kutoka katika mechi hii ilikuwa ni kashfa nyingine ya tukio la Luiz Suarez ‘kung’ata’

Mshambulizi huyo wa Liverpool alionekana kumng’ata beki wa Juventus Giorgio Chiellini dakika moja kabla ya Diego Godin kufungia Uruguay bao la ushindi.

Mapema katika mechi hiyo, kiungo cha kati wa Italia Claudio Marchisio alikuwa ameonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Egidio Arevalo.

Uruguay sasa itacheza dhidi ya Colombia au Ivory Coast jijini Maracana siku ya Jumamosi katika raundi ya pili ya Kombe la Dunia, lakini utata unatarajiwa kuibuka kabla ya siku hiyo.

Italia walitoka uwanjani wakiwa na ghadhabu kutokana na waliyoshuhudia kabla yao kuondolewa katika kombe la Dunia la pili bila kupita kutoka mechi za makundi- kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 1966.

Kocha wa Italia Cesare Prendelli alisema kabla ya mchezo kuwa ilikuwa “mechi muhimu sana katika taaluma yake kandanda” na baada ya kushindwa akapendekeza kujiuzulu.

Mechi hii ilikuwa na hamaki na hasira ndani na nje ya uwanja.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Baloteli hakuvuma katika mechi hii

Mara kwa mara wasaididizi wa refari walilazimika kuzuia zogo kati ya timu hizo mbili, kipenga cha refarii kikatiza mchezo mara nyingi na wachezaji wakachukua muda mrefu wakisukumana walipokuwa wakikimbia na mpira miguuni.

Italia ilikuwa ikihitaji sare tu ili kufuzu. Katika mfumo wa 3-5-2, Italia walikosa mshikamano, mbio na walihatarisha lango lao kila wakati. Lakini iwapo mfumo wao ulitekelezwa ili kuzuia ushambulizi wa Uruguay, mfumo huo ulisaidia.

Andrea Pirlo alimlazimu mlindalango wa Uruguay Fernando Muslera kuondoa mkwaju wake uliotokana na mpira wa adhabu na kuugongesha mlingoti, huku mshambulizi Ciro Immobile akipiga mkwaju nje ya lango.

Edinson Cavani alitaka kuzawadiwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 50 baada ya kuangushwa na Andrea Barzagli, lakini refarii akapuuzilia mbali.

Refarii huyo raiya wa Mexico hata hivyo angebadili mchezo muda mfupi baadae wakati alipomwonyesha Marchisio kadi nyekundu baada ya kiungo huyo wa kati wa Juventus kumchezea vibaya Arevalo katikati mwa uwanja.

Marchisio alinyanyua mguu na kumgonga kiungo huyo wa Uruguay gotini.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Chiellini akimwonesha refarii alikongatwa na Suarez

Suarez alikaribia kufunga bao alipopiga mkwaju wa chini kwa chini ambao Buffon aliudaka .

Utata zaidi ulizuka wakati Suarez na Chiellini walipokumbana katika maeneo ya penalti zikiwa zimesalia dakika tisa kwa mechi kukamilika.

Beki huyo wa Italia alilalamika wakati huo huo kwa refarii kwamba alikuwa ameng’atwa na akajaribu kumwonyesha alama.

Wakati wachezaji wa Italia walipokuwa wakiendelea kulalamika, Uruguay wakapata kona.

Suarez alipiga pasi nzuri naye Godin akafunga bao hilo la ushindi.

Itali walijaribu kila wawezalo ili kupata bao, hadi mlindalango Buffon kujaribu kutafuta bao kutokana na kona waliyopata waitaliano dakika za mwisho, lakini upande wake Oscar Tabarez ukawadhibiti.

Hata hivyo huenda mechi hii isikumbukwe sana. Macho yote, kwa mara nyingine yatamwelekea Suarez.