Wachezaji wa Ghana walipwa fedha zao

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa Ghana

Serikali ya Ghana imetuma dola millioni 3 nchini Brazil ili kuwalipa wachezaji wake wa soka fedha za kushiriki katika michuano hiyo wanazodai.

Naibu Spika Joseph Yamin ameiambia radio ya Citi Fm nchini humo kwamba,''wachezaji wamesisitiza kwamba ni sharti wapewe fedha hizo taslimu .

''Serikali ililazimika kutafuta fedha hizo na kuzituma kupitia usafiri wa ndege hadi brazil.Fedha hizo ni zaidi ya millioni 3''.

Ghana ni sharti iishinde Ureno siku ya alhamisi ili kujikatia tiketi ya kuendelea kushiriki katika michuano hiyo.

Iwapo itashindwa ama kutoka sare yoyote basi itakuwa imebanduliwa katika mashindano hayo,na iwapo watashinda na Ujerumani na Marekani kutoka sare katika mechi nyengine ya kundi G basi watakuwa wametolewa.

Mapema juma hili kulikuwa na madai kwamba timu hiyo ya Black Stars ilikuwa ikipanga kugoma iwapo hawatalipwa fedha hizo.

Na huku wasiwasi ukiendelea katika kambi ya timu hiyo ,rais wa Ghana John Dramani Mahama yeye mwenyewe aliingilia kati na kuwaahidi wachezaji hao kwamba watalipwa fedha zao.

Taarifa kutoka shirikisho la soka la Ghana ilisema;''Serikali inawalipa wachezaji wa timu hiyo fedha za kushiriki katika michuano ya kombe la dunia na fedha hizo zitarudishwa wakati shirikisho la soka duniani FIFA litakapolipa fedha za kushiriki katika mechi hizo baada ya kukamilika kwa michuano hiyo''.